Rais Dkt.Samia awataka viongozi kutafsiri vipaumbele vya Serikali

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa Serikali kufanya kazi kwa bidii, kusimamia vipaumbele vya Serikali na kuhakikisha dhamana wanazopewa zinaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Elias Magembe akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Ndugu Charles Ngeleja Kandonya pamoja na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Ndugu Nolasco Jacob, wakiapa Kiapo cha Maadili, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 01 Julai, 2026.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Ikulu, Dar es Salaam, baada ya kuwaapisha viongozi wapya aliowateua hivi karibuni katika nafasi mbalimbali za utumishi wa umma.

“Dhamana mlizopewa ni zaidi ya vyeo. Nendeni mkazitendee haki kwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu, mkiwatumikia wananchi,” amesema Rais Dkt. Samia.

Amewataka viongozi hao kusukuma vipaumbele vya Serikali kwa kasi na matokeo, akisema wanaanza kazi wakati Serikali ikianza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/2027.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Ndugu Nolasco Jacob Kipanda kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 01 Julai, 2026.

Katika sekta ya afya, Rais Dkt. Samia amesisitiza usimamizi makini wa bajeti, vipaumbele na rasilimali zilizopo ili huduma ziwafikie wananchi kwa haraka na kwa ubora unaotakiwa.

Amesema Serikali inalenga kuongeza uzalishaji wa dawa, vifaa tiba na chanjo nchini ili kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje, kuongeza upatikanaji wa huduma za afya nchini, na kubana matumizi ya fedha za nchi katika uagizaji wa bidhaa hizo.

“Lengo letu ni kufikia angalau asilimia 60 ya uzalishaji wa ndani wa dawa, vifaa tiba na chanjo ifikapo mwaka 2030. Wakaribisheni wawekezaji kwenye eneo hili, lakini kwa kuzingatia ubora,” amesema Rais Dkt. Samia.

Akizungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuendelea kusimamia maslahi ya Tanzania katika biashara, uchumi na fursa za maendeleo, na kuimarisha Jumuiya hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka, Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi kwenye picha na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Elias Magembe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Ndugu Charles Ngeleja Kandonya, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Ndugu Nolasco Jacob, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 01 Julai, 2026.

Aidha, Rais Dkt. Samia ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kusimamia mashauri, malalamiko na migogoro ya watumishi kwa uwazi na haki, ili kuendelea kujenga nidhamu,uadilifu na imani katika utumishi wa umma.

Viongozi walioapishwa ni Dkt. Grace Elias Magembe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya; Bw. Charles Ngeleja Kadonya kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki; na Bw. Nolasco Jacob Kipanda kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here