NA DIRAMAKINI
KUFUATIA mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Daniel Francisco Chapo Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 02 hadi 04 Julai,2026.
Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Rais Chapo anatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mazungumzo hayo yatajikita katika kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, uchukuzi, nishati pamoja na kuangazia maeneo mapya ya ushirikiano yenye maslahi ya pamoja kwa wananchi wa nchi hizi mbili.
Mnamo tarehe 03 Julai 2026, Mheshimiwa Rais Chapo anatarajiwa kufungua rasmi Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba, yatakayowakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.
Aidha, Mheshimiwa Rais Chapo atamtembelea Mama Maria Nyerere, Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa lengo la kutoa heshima na kutambua mchango wa viongozi waasisi katika kuimarisha uhusiano wa kindugu kati ya Tanzania na Msumbiji, hususan wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.
Ziara ya Mheshimiwa Rais Chapo ni kielelezo cha uhusiano imara wa kihistoria na ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na Msumbiji, na inatarajiwa kuendelea kufungua fursa mpya za ushirikiano katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Itakumbukwa kuwa, ziara hii ni ya tatu kwa Mheshimiwa Rais Chapo nchini Tanzania tangu alipoingia madarakani mwaka 2024, jambo linaloakisi dhamira ya viongozi wa nchi hizi mbili ya kuendelea kuimarisha mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa karibu, yaliyojengwa juu ya historia ya ujirani mwema na mshikamano wa muda mrefu.

