NA GODFREY NNKO
TANZANIA imeandika historia kwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuandaa Mkutano wa Nne wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuhusu Utabiri wa Hali ya Hewa wa Kiutendaji (Operational Climate Prediction-OCP-4), huku Serikali ikisisitiza matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence-AI) katika kuimarisha mifumo ya utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za mapema kwa ajili ya kuokoa maisha, kulinda miundombinu na kukuza uchumi.
Mkutano huo wa siku tatu ulioanza Juni 29, 2026 katika Ukumbi wa Papu Tower jijini Arusha umewakutanisha wataalamu wa hali ya hewa kutoka Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na mamlaka za hali ya hewa kutoka zaidi ya nchi 30.Akifungua mkutano huo, Waziri wa Uchukuzi,Profesa Makame Mbarawa amesema, Tanzania imepewa heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo katika kipindi ambacho Afrika inaendelea kukabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mafuriko, ukame na vimbunga vinavyoongezeka kwa kasi.
Amesema,matukio hayo yanaendelea kuhatarisha maisha ya wananchi, miundombinu pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika sayansi ya utabiri wa hali ya hewa na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Profesa Mbarawa amewataka wataalamu kutumia uwezo wa Akili Unde (AI) na teknolojia za kujifunza kwa mashine (Machine Learning) kuboresha mifumo ya utabiri wa hali ya hewa ili kutoa taarifa sahihi na zinazoweza kutumika katika kufanya maamuzi kwa wakati.Ameeleza kuwa, sekta ya uchukuzi ni miongoni mwa sekta zinazotegemea kwa kiwango kikubwa taarifa sahihi za hali ya hewa.
“Usafiri wa anga, baharini na nchi kavu unategemea kwa kiasi kikubwa hali ya hewa. Utabiri sahihi ni muhimu katika kulinda usalama wa wasafiri, kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji na kulinda miundombinu muhimu ya taifa,”amesema.
Waziri huyo pia ameeleza kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeongeza uwekezaji katika sekta ya hali ya hewa kwa kuongeza bajeti na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati.
Miradi hiyo ni pamoja na ununuzi na ufungaji wa rada za kisasa za hali ya hewa, ujenzi wa Kituo cha Vifaa vya Hali ya Hewa jijini Dar es Salaam, ujenzi wa Kituo Kipya cha Kitaifa cha Utabiri wa Hali ya Hewa pamoja na kuimarisha mifumo ya uchunguzi wa anga.
Aidha, amesema Tanzania inaendelea kutekeleza programu za kimataifa zinazoratibiwa na WMO, zikiwemo Systematic Observation Financing Facility (SOFF) na Early Warnings for All (EW4All), ambazo zinalenga kuboresha mifumo ya utabiri na utoaji wa tahadhari za mapema kuhusu majanga ya asili.Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Kinyasi Millya amewakaribisha wajumbe nchini Tanzania na kueleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na WMO ulianza mwaka 1962.
Amesema, Tanzania imeendelea kunufaika na programu mbalimbali za kimataifa zinazolenga kuimarisha huduma za hali ya hewa na kwamba ushirikiano wa kikanda ni muhimu kwa kuwa majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi hayaheshimu mipaka ya nchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt.Ladislaus Chang'a, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) amesema,mkutano huo unafanyika wakati ambapo dunia imeshuhudia miaka mitatu mfululizo ikiwa ya joto zaidi kuwahi kurekodiwa.
Ameonya kuwa bila kuimarisha mifumo ya utabiri wa hali ya hewa, jamii zinazotegemea sekta nyeti kama kilimo, maji na uchukuzi zitaendelea kuathirika na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Dkt.Chang'a pia amesema,Tanzania imeendelea kuwa kinara katika kuzijengea uwezo nchi mbalimbali duniani ikiwemo Nigeria, Libya, Namibia, Lesotho, Burundi na Sudan Kusini katika mifumo ya ubora wa huduma za hali ya hewa na utabiri wa matukio makubwa ya hali mbaya ya hewa.
Mkutano wa OCP-4 unafanyika baada ya mikutano ya awali kufanyika Pune nchini India mwaka 2015, Barcelona nchini Hispania mwaka 2018 na Lisbon nchini Ureno mwaka 2022, hatua inayoonesha kuongezeka kwa nafasi ya Afrika katika utafiti na maendeleo ya sayansi ya hali ya hewa duniani.
Washiriki wa mkutano huo wanajadili namna ya kutumia Akili Unde, utabiri wa pamoja (ensemble forecasting) pamoja na utabiri wa hali ya hewa wa msimu hadi miaka kadhaa ijayo ili kuboresha huduma zinazowanufaisha wakulima, sekta ya uchukuzi na taasisi zinazoshughulikia usimamizi wa maafa.Akihitimisha hotuba yake, Profesa Mbarawa amewataka wajumbe kutumia mkutano huo kubadilishana uzoefu na kubuni suluhisho za kisayansi zitakazosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ustahimilivu wa jamii.
Tags
Habari
Kimataifa
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania










