NA GODFREY NNKO
JIJI la Arusha limeandika historia kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nne wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuhusu Utabiri wa Hali ya Hewa wa Kiutendaji (Operational Climate Prediction-OCP-4), ikiwa ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika barani Afrika tangu ulipoanzishwa miaka 11 iliyopita.
Mkutano huo umewakutanisha zaidi ya wataalamu 200 wa hali ya hewa, wanasayansi, wataalamu wa Akili Unde (Artificial Intelligence-AI), mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wa maendeleo kutoka zaidi ya mataifa 30 kujadili namna ya kutumia teknolojia za kisasa kutabiri majanga ya asili kabla hayajatokea na kupunguza athari zake kwa wananchi.
Akifungua mkutano huo Juni 29, 2026, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema, mabadiliko ya tabianchi si suala la mazingira pekee bali yamekuwa na athari kubwa kwa uchumi, usafiri, biashara na utalii.
Ameeleza kuwa,sekta ya uchukuzi ndiyo inayotegemea kwa kiwango kikubwa taarifa sahihi za hali ya hewa.
“Usafiri wa anga, baharini na nchi kavu unaathirika moja kwa moja na hali ya hewa. Utabiri sahihi ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa wasafiri, kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji na kulinda miundombinu muhimu ya taifa,”amesema Profesa Mbarawa.
Kauli hiyo imekuja wakati Tanzania ikiendelea kuwekeza katika Reli ya Kisasa (SGR), ambayo inapita katika maeneo yanayoweza kuathiriwa na mafuriko makubwa endapo hakutakuwa na mifumo madhubuti ya utabiri wa hali ya hewa.
AI yabadilisha Sayansi ya Utabiri
Moja ya ajenda kuu za mkutano huo ni matumizi ya Akili Unde (AI), teknolojia ya kujifunza kwa mashine (Machine Learning), utabiri wa pamoja (Ensemble Forecasting) na uchambuzi wa data kubwa (Big Data) katika kuboresha usahihi wa utabiri wa hali ya hewa.
Badala ya mifumo ya kawaida ya kutoa makadirio ya jumla ya mvua, teknolojia hizo zinatarajiwa kuwezesha utabiri wa maeneo mahususi wiki kadhaa kabla ya tukio kutokea.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ladislaus Chang'a, anasema,maendeleo makubwa yamepatikana katika sayansi ya utabiri wa hali ya hewa, lakini changamoto kubwa iliyobaki ni kuhakikisha taarifa hizo zinawafikia wananchi kwa lugha rahisi na kwa wakati.
"Mahitaji ya taarifa za hali ya hewa zilizo sahihi, zinazotegemewa na zinazoweza kutumika katika kufanya maamuzi yanaongezeka kila siku, hasa kwa jamii zilizo katika mazingira hatarishi,”amesema Dkt. Chang'a.
Ameongeza kuwa,bila kuimarisha huduma za utabiri, sekta nyeti kama kilimo, maji, uchukuzi na usimamizi wa maafa zitaendelea kuathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Serikali yaongeza uwekezaji
Katika jitihada za kuimarisha huduma za hali ya hewa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kuongeza bajeti ya sekta hiyo kwa miaka mitano mfululizo.
Profesa Mbarawa anasema,fedha hizo zimeelekezwa katika miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ununuzi na ufungaji wa rada za kisasa za hali ya hewa, ujenzi wa Kituo cha Vifaa vya Hali ya Hewa jijini Dar es Salaam, ujenzi wa Kituo Kipya cha Kitaifa cha Utabiri wa Hali ya Hewa pamoja na kuimarisha mifumo ya uchunguzi wa anga.
Aidha, Tanzania inaendelea kutekeleza programu za kimataifa za Systematic Observation Financing Facility (SOFF) na Early Warnings for All (EW4All) zinazolenga kuboresha uwezo wa kutoa tahadhari za mapema kuhusu majanga ya asili.Tanzania kitovu cha maarifa Afrika
Mbali na kunufaika na ushirikiano wa kimataifa tangu kujiunga na WMO mwaka 1962, Tanzania sasa imeanza kutoa utaalamu kwa mataifa mengine.
Kwa mujibu wa Dkt. Chang'a, TMA imefanikiwa kusaidia nchi mbalimbali ikiwemo Nigeria, Libya, Namibia, Lesotho, Burundi na Sudan Kusini kuimarisha mifumo yao ya utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za mapema.
Hatua hiyo imeifanya Tanzania kuwa moja ya vituo muhimu vya maendeleo ya sayansi ya hali ya hewa katika nchi za Kusini mwa Dunia.
Ushirikiano wa Kimataifa ni muhimu
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Kinyasi Millya, amesema,majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi hayaheshimu mipaka ya nchi, hivyo ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni muhimu katika kukabiliana nayo.
Amesema,Tanzania inatumia mkutano huo kuendeleza ajenda za kimataifa ikiwemo Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Mfumo wa Sendai wa Kupunguza Athari za Maafa.
Kwa nini wananchi wanapaswa kujali?
Wataalamu wanasema manufaa ya teknolojia hizo hayatabaki kwa taasisi za kisayansi pekee. Kwa mfano mkulima wa Singida, utabiri sahihi unaweza kumwezesha kupanga msimu wa kilimo kwa usahihi na kupunguza hasara.
Vilevile,kwa dereva wa malori, taarifa za mapema zinaweza kusaidia kupanga safari salama na kuepuka maeneo yenye mafuriko au maporomoko ya ardhi.
Kwa sekta ya uchukuzi, utalii na biashara, mifumo hiyo itasaidia kupunguza athari za majanga na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi.
Arusha yatuma ujumbe kwa Dunia
Kufanyika kwa OCP-4 nchini Tanzania kunaonesha kuongezeka kwa nafasi ya Afrika katika utafiti wa sayansi ya hali ya hewa na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Mkutano huo unatoa ujumbe kuwa,Tanzania haitaki tena kusubiri majanga yatokee ndipo ichukue hatua, bali inalenga kuyatabiri mapema, kuyapangia mikakati na kupunguza athari zake kwa wananchi na uchumi wa taifa.
Kwa sasa, macho ya dunia yanaelekezwa Arusha, ambako wataalamu wanaendelea kujadili namna ya kutumia Akili Unde na sayansi ya hali ya hewa kujenga jamii salama zaidi na yenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Tags
Habari
Makala
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania








