NA DIRAMAKINI
KAMATI ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (MPC) imesema,bei za vyakula zinatarajiwa kupungua katika nusu ya pili ya mwaka 2026 kutokana na mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa mwaka 2025/26, huku thamani ya Shilingi ikitarajiwa kuendelea kuimarika kutokana na kuongezeka kwa mapato ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba ameyasema hayo leo Julai 3,2026 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam wakati akitangaza Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa Robo ya Tatu ya Mwaka 2026.
Ni katika mkutano uliohudhuriwa na viongozi wa benki,taasisi za fedha na waandishi wa habari nchini ambapo amesema, hali hiyo itasaidia kupunguza gharama za maisha na kudhibiti mfumuko wa bei.
"Hali hii itasaidia kupunguza bei za chakula na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, na hivyo kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo katika nusu ya pili ya mwaka 2026,"amesema Gavana Tutuba.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Sera ya Fedha imeongeza kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia 5.75 hadi asilimia 6.25 kwa robo ya tatu ya mwaka 2026, kuanzia Julai hadi Septemba.
Gavana Tutuba amesema,uamuzi huo umetokana na ongezeko la shinikizo la mfumuko wa bei linalochochewa na kupanda kwa bei za mafuta, mbolea na gharama za usafirishaji duniani kutokana na mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.
"Kamati imeona kuwa ongezeko hili la Riba ya Benki Kuu ni sahihi katika kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5, huku ikiendelea kuunga mkono ukuaji wa shughuli za uchumi,"amesema.
Pia,amesema licha ya changamoto za kiuchumi zinazotokana na mazingira ya kimataifa, uchumi wa Tanzania umeendelea kuonesha uimara.
Kwa mujibu wa BoT, uchumi wa Tanzania Bara unakadiriwa kukua kwa asilimia sita katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, ukichochewa na ukuaji wa sekta za kilimo, ujenzi, madini, huduma za kifedha na usafirishaji.
Aidha, uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.6, ukichangiwa zaidi na kuimarika kwa sekta za utalii na ujenzi.
Kuhusu mfumuko wa bei, Gavana Tutuba amesema kwa Tanzania Bara uliongezeka hadi asilimia 4.2 mwezi Mei 2026 kutoka asilimia 3.2 mwezi Machi, lakini umeendelea kubaki ndani ya lengo la Benki Kuu la asilimia 3 hadi 5.
Ameeleza kuwa,ruzuku ya mafuta iliyotolewa na Serikali katika miezi ya Mei na Juni mwaka huu imechangia kupunguza kasi ya ongezeko la mfumuko wa bei.
Kwa upande wa Zanzibar, Gavana Tutuba amesema,mfumuko wa bei uliongezeka hadi asilimia 5.5 mwezi Mei kutoka asilimia 4.9 mwezi Machi, lakini bado unatarajiwa kurejea katika kiwango kinacholengwa kadri mazingira ya uchumi yatakavyoendelea kuimarika.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa uongozi wake katika kusimamia sera za fedha zinazowezesha uchumi wa Tanzania kuendelea kukua licha ya changamoto zinazotokana na migogoro ya kisiasa na kiuchumi duniani.
Sabi amesema ushirikiano unaoendelea kati ya Benki Kuu na sekta ya fedha umechangia kuimarisha mfumo wa kifedha nchini na kuweka mazingira mazuri ya kukuza uwekezaji, biashara na maendeleo ya uchumi kwa ujumla.
Wakati huo huo,kamati pia imeeleza kuwa,hali ya ukwasi nchini iliendelea kuwa tulivu katika robo ya pili ya mwaka 2026, huku mikopo kwa sekta binafsi ikikua kwa wastani wa asilimia 24 kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji.
Sekta ya benki pia iliendelea kuwa imara, yenye faida na mtaji wa kutosha kukabiliana na misukosuko ya kifedha, huku kiwango cha mikopo chechefu kikibaki asilimia 2.9 mwezi Mei 2026, chini ya kiwango cha juu kinachokubalika cha asilimia 5.
Benki Kuu imesema,akiba ya fedha za kigeni imefikia takribani dola za Marekani bilioni 6, kiwango kinachotosheleza kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.3, juu ya lengo la taifa la angalau miezi minne.
Aidha, akiba hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi kutokana na mauzo ya bidhaa nje ya nchi pamoja na ununuzi wa dhahabu kutoka kwa wazalishaji wa ndani.

