Uchunguzi wa kisayansi waanza kifo cha dereva wa John Heche

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi Mkoa wa Kigoma limesema linaendelea na uchunguzi wa kisayansi kuhusu kifo cha Suezi Dani Maradufu, mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye alikuwa dereva wa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche huku sampuli mbalimbali zikichukuliwa ili kubaini chanzo halisi cha kifo chake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philimon Makungu ameyaeleza hayo katika taarifa iliyotolewa Julai 3,2026.

Ameeleza kuwa,uchunguzi wa awali wa mwili wa marehemu umefanywa na jopo la madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Bugando, wakishirikiana na wataalamu wa afya kutoka mikoa ya Geita na Dodoma pamoja na Afisa Mwandamizi kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Amesema,uchunguzi huo ulifanyika mbele ya ndugu wa marehemu pamoja na viongozi wa CHADEMA ili kuhakikisha uwazi katika mchakato wa uchunguzi.

Kwa mujibu wa Kamanda Makungu, wataalamu walichukua sampuli mbalimbali kutoka katika mwili wa marehemu ambazo zitafanyiwa uchunguzi wa kina wa kisayansi ili kuthibitisha chanzo halisi cha kifo.

Ameeleza kuwa,matokeo ya uchunguzi huo yatakapokamilika yataisaidia mamlaka husika kubaini mazingira na sababu za kifo hicho.

Suezi Dani Maradufu alifariki Julai 1, 2026 akiwa ndani ya chumba alichokuwa amepanga katika nyumba ya kulala wageni ya Ntahamba, mkoani Kigoma.

Kifo chake kimeibua mjadala miongoni mwa wananchi na viongozi wa kisiasa, huku CHADEMA ikitaka kufanyika kwa uchunguzi huru na wa kina ili kubaini mazingira yaliyosababisha kifo hicho.

Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa,uchunguzi unaendelea kwa kuzingatia taratibu za kisayansi na kisheria, na limewataka wananchi kuwa na subira pamoja na kuepuka kutoa hitimisho kabla ya matokeo rasmi ya uchunguzi kutolewa na mamlaka husika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here