Dawa za kulevya zinaua ndoto na vizazi, tuzikatae wote-DCEA

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewataka waandishi wa habari nchini kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha umma kuhusu tishio linaloongezeka la matumizi yasiyo sahihi ya kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya, ikisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuzuia kuenea kwa tatizo hilo.
Wito huo umetolewa Julai 3, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya, iliyolenga kuongeza uelewa wa wanahabari kuhusu mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu pamoja na athari za matumizi ya dawa hizo.

Akizungumza katika semina hiyo, Mfamasia Mkuu wa DCEA, Upendo Chenya amesema, matumizi ya dawa za kulevya na dawa tiba zenye asili ya kulevya yanaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya jamii na maendeleo ya Taifa, huku athari zake zikiendelea kujitokeza hata kwa vizazi vijavyo.

Amesema,uraibu wa dawa za kulevya huwanyima watumiaji nafasi ya kuishi maisha yenye afya na kushuhudia ukuaji wa vizazi vyao kutokana na madhara makubwa yanayosababishwa na matumizi ya dawa hizo.
"Matumizi ya dawa za kulevya yana athari kubwa kwa familia na jamii. Tunahitaji kujenga jamii isiyokuwa tegemezi kwa dawa za kulevya ili kulinda nguvu kazi ya Taifa na mustakabali wa vizazi vijavyo,"amesema Chenya.

Ameongeza kuwa,uelewa mdogo kuhusu matumizi mabaya ya kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya umechangia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaoingia kwenye utegemezi wa dawa hizo duniani.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), zaidi ya watu milioni 331 duniani wanatumia dawa za kulevya, huku takribani milioni 63 wakikumbwa na madhara yanayohitaji matibabu. Aidha, nchini Tanzania, zaidi ya watu 62,000 wameripotiwa kutafuta huduma za matibabu ya uraibu.

Pia, UNODC inakadiria kuwa ifikapo mwaka 2030 idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya barani Afrika itaongezeka kwa asilimia 40, wakati duniani ongezeko linatarajiwa kufikia asilimia 11.

"Matumizi ya dawa za kulevya yanatukosesha kushuhudia kizazi cha pili, cha tatu na cha nne hivyo dawa za kulevya ni mfano wa kitu ambacho kinawekwa duniani ili kuwaondoa watu kwenye mfumo wa kuishi kama Mungu alivyomkusudia kila mmoja wetu."

Katika semina hiyo, Kamishna Msaidizi wa Uchunguzi wa DCEA, Ziliwa Machibya amesema,matumizi ya kemikali bashirifu katika utengenezaji wa dawa za kulevya yamekuwa yakiongezeka duniani, jambo linalohitaji usimamizi madhubuti wa sheria na ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Amesema mwaka 2025, DCEA ilikamata tani 31.76 na lita 183,500 za kemikali bashirifu, huku tani nyingine 734 zikizuiwa kuingia nchini kinyume cha sheria.

Machibya amesema,kemikali hizo hudhibitiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kemikali za Viwandani na Majumbani (Udhibiti na Usimamizi) Na.3 ya mwaka 2003, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015 pamoja na Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba.

Sambamba na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1988 wa kudhibiti usafirishaji haramu wa dawa za kulevya na kemikali bashirifu.

Amefafanua kuwa,kemikali zinazodhibitiwa ni pamoja na acetone, ethanol, hydrochloric acid, methylamine, benzyl alcohol, toluene na nyinginezo ambazo hutumika kuzalisha dawa mbalimbali za kulevya.

Akitoa mifano ya matukio yaliyobainika nchini, amesema DCEA iliwahi kubaini kilo 12 za kemikali aina ya pseudoephedrine zilizochepushwa wakati wa utengenezaji wa dawa za kikohozi, hali iliyosababisha kuharibiwa kwa lita 10,000 za dawa zilizokuwa na kiwango pungufu cha kiambata hicho.

Vilevile amesema,uchunguzi mwingine uliwezesha kubaini usafirishaji wa tani 21.7 za kemikali aina ya acetic anhydride kutoka Tanzania kwenda Pakistan kwa kutumia jina bandia la acetic acid, pamoja na kuzuiwa kwa tani nne za kemikali zilizokuwa zielekezwe Mexico kutengeneza dawa ya kulevya aina ya fentanyl kwa kutumia jina bandia la protein biotine.
Machibya pia amesema,uchunguzi wa pamoja uliwezesha kubaini maabara bubu ya kutengeneza dawa ya kulevya aina ya methamphetamine katika eneo la Namanga upande wa Kenya, jambo lililoonesha umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.

Akizungumzia dawa tiba zenye asili ya kulevya, amesema dawa hizo si dawa za kulevya zenyewe bali ni dawa halali zinazotumika hospitalini kwa ajili ya matibabu chini ya usimamizi wa wataalamu wa afya.

"Hizi ni dawa muhimu kwa matibabu. Tatizo huanza pale zinapochepushwa kutoka katika matumizi yake halali na kutumika kutengeneza au kuchanganywa na dawa za kulevya,"amesema.

Ameongeza kuwa,matumizi mabaya ya dawa hizo husababisha uraibu,utegemezi, magonjwa ya akili, matatizo ya mfumo wa upumuaji, kuharibika kwa viungo vya mwili, kupoteza hamu ya kula na hata vifo vya ghafla.

Kwa wanawake wajawazito, Machibya amesema matumizi hayo yanaweza kusababisha kuharibika kwa mimba, kujifungua watoto wenye uzito mdogo na kuathiri afya ya kizazi kijacho.
Kwa upande wa athari za kijamii na kiuchumi, Machibya amesema uchepushaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya huchochea uhalifu, huongeza gharama za huduma za afya, hupunguza upatikanaji wa dawa muhimu kwa wagonjwa na kuilazimu Serikali kutumia rasilimali nyingi katika matibabu ya waraibu pamoja na operesheni za kudhibiti biashara hiyo.

Machibya amewahimiza waandishi wa habari kutumia maarifa waliyopata katika semina hiyo kuandika habari zenye kuelimisha umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya, mbinu zinazotumiwa na wahalifu na umuhimu wa kuzingatia sheria katika udhibiti wa kemikali bashirifu, akisisitiza kuwa vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kulinda afya na usalama wa jamii nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here