Uwekaji wa jiwe la msingi la SGR Tabora hadi Kigoma:Mwanzo wa fursa mpya kwa Kigoma

KIGOMA-Julai 20,2026 itaendelea kukumbukwa kama siku muhimu katika historia ya maendeleo ya Mkoa wa Kigoma, kufuatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha sita kutoka Tabora hadi Kigoma.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu,taarifa iliyotolewa leo na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha Shirika la Reli Tanzania (TRC) imeeleza kuwa, hatua hii si tukio la uwekaji wa jiwe la msingi pekee, bali ni ishara ya dhamira ya Serikali ya kuunganisha Kigoma na mtandao wa kisasa wa usafiri, biashara na maendeleo ya Taifa.

Kiuchumi, reli ya SGR inatarajiwa kuibadilisha Kigoma kuwa lango muhimu la biashara kwa ukanda wa Maziwa Makuu.

Kupitia reli hii, usafirishaji wa bidhaa kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Kigoma utakuwa wa haraka, salama na wenye gharama nafuu.

Hali hiyo itaongeza ushindani wa biashara, kuvutia wawekezaji, kuchochea viwanda, na kuimarisha biashara na nchi jirani kama Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Kongo (DRC), ambazo zinategemea kwa kiasi kikubwa Ushoroba wa Kati.

Kijamii, reli hii itarahisisha usafiri wa wananchi, kupunguza muda wa safari na kuongeza upatikanaji wa huduma mbalimbali.

Urahisi wa usafiri utachochea ukuaji wa sekta za utalii, elimu, afya na biashara ndogondogo, huku ukifungua fursa mpya za ajira na kuongeza kipato cha wananchi wa Kigoma na maeneo jirani.

Aidha, utekelezaji wa mradi huu unatoa nafasi kubwa ya kuimarisha local content, yaani ushiriki wa Watanzania katika shughuli za ujenzi na uendeshaji wa mradi.

Hii inajumuisha ajira kwa wananchi wa maeneo yanayopitiwa na reli, ushiriki wa wakandarasi na wasambazaji wa ndani, pamoja na uhamishaji wa ujuzi na teknolojia kwa wahandisi, mafundi na wataalamu wa Kitanzania.

Matokeo yake ni kujenga uwezo wa ndani ambao utaendelea kunufaisha Taifa hata baada ya mradi kukamilika.

Kwa ujumla, uwekaji wa jiwe la msingi la SGR Tabora–Kigoma, ni hatua ya kimkakati inayobeba matumaini mapya kwa wananchi wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla.

Ni uwekezaji unaolenga kuunganisha watu, masoko na fursa za maendeleo, huku ukiweka msingi wa uchumi shindani, jumuishi na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here