Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT) laendelea kuwa nguzo muhimu utatuzi wa migogoro

DODOMA-Baraza la Masoko ya Mitaji (Capital Markets Tribunal-CMT) linaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha uendelevu wa upatikanaji wa haki kwa haraka na weledi katika utatuzi wa migogoro inayohusu masoko ya mitaji, dhamana na biashara ya bidhaa nchini.
Likiwa na mamlaka sawa na Mahakama Kuu katika kushughulikia mashauri ya madai yanayohusu masoko ya mitaji, dhamana na bidhaa; Baraza hilo, ni chombo huru cha kisheria kilichoanzishwa chini ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Sura ya 79.

Akizungumza wakati akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT) kwenye Manoesho ya Nane Nane 2026, lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Fedha, Msajili wa Baraza la Masoko ya Mitaji Tanzania (CMT), Mhe. Dkt. Martin Wilbert Kolikoli, alisema Baraza hilo linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kukuza uchumi wa nchi.

‘’Lengo kuu la kuanzishwa kwa Baraza hii ni kuhakikisha migogoro inayojitokeza katika sekta ya masoko ya fedha inashughulikiwa kwa haraka, kwa haki na kwa kutumia utaalamu maalumu unaozingatia mazingira ya sekta hiyo hivyo tunahakikisha kuwa kwa pamoja tunajenga masoko ya haki, yenye tija katika na kuwa endelevu kuelekea Dira 2050,’’ alisema Dkt. Kolikoli.
Alisema, uwepo wa Baraza hilo unachangia kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ulinzi wa haki za washiriki wa masoko ya mitaji, huku ukiunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza uchumi kupitia sekta ya fedha na uwekezaji.

‘’Lengo letu ni kuongeza imani na ujasiri katika sekta ya kilimobiashara; kuwawezesha wakulima, vyama vya ushirika na wajasiriamali wa kilimo kutumia kikamilifu na kunufaika na masoko yetu ya bidhaa na hisa, pamoja na mipango ya uwekezaji wa pamoja,’’ alisema Dkt. Kolikoli.

Alieleza kuwa, CMT inatekeleza jukumu la kusikiliza na kuamua migogoro inayotokana na shughuli za Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) pamoja na Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (Collective Investment Schemes).
Aliongeza kuwa,Baraza hilo lina mamlaka ya kushughulikia mashauri yanayohusu hisa, hati fungani za kampuni, vipande vya uwekezaji (units), mifuko ya uwekezaji inayouzwa sokoni (Exchange Traded Funds-ETFs), pamoja na biashara ya mazao inayofanyika kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Uuzaji wa TMX.

Alibainisha kuwa, Baraza hilo linaongozwa na Mwenyekiti ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, akisaidiwa na wajumbe wanne wenye utaalamu katika masuala ya sheria na masoko ya mitaji. Shughuli zake za kila siku zinaratibiwa na Sekretarieti inayoongozwa na Msajili.

Moja ya sifa zinazotofautisha Baraza la Masoko ya Mitaji ni kasi ya utoaji wa haki ambapo baada ya usikilizwaji wa shauri kuanza, mchakato mzima wa kulisikiliza na kuliamua hukamilika ndani ya siku 45, hatua inayosaidia kupunguza ucheleweshaji wa mashauri na kuongeza imani ya wawekezaji na wadau wa sekta ya fedha.
Maadhimisho ya Nane Nane 2026 yenye kaulimbiu ‘’Tambua soko ongeza tija kuendeleza Dira 2050, ni Maadhimisho ya 33 ambayo yanalenga kukuza uchumi, kuongeza matumizi ya teknolojia bora na kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa ambayo yanaendelea katika Uwanja wa Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here