NA DIRAMAKINI
KATIKA kipindi ambacho imeshuhudiwa katika kona mbalimbali Dunia ikikabiliwa na changamoto kubwa za mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu pamoja na mahitaji makubwa ya huduma za majisafi na salama, Tanzania imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha Sekta ya Maji kupitia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Taswira ya mradi wa bwawa la Kidunda, mradi ambao wazo lake lilianza miaka 50 iliyopita ambapo hivi sasa linatekelezwa na Serikali kwa fedha za ndani zaidi ya shillingi bilioni 300, ujenzi wake umefika asilimia 52.4. Bwawa hili litakuwa muarobaini katika kuimarisha huduma yam aji kwa mikoa ya Dar es salaam na Pwani, pamoja na maeneo jirani.
Miongoni mwa viongozi waliojitokeza kwa nguvu katika kusukuma ajenda hiyo ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ambaye amekuwa mstari wa mbele kutumia Diplomasia ya Kimataifa kutafuta washirika na wawekezaji wapya katika sekta hiyo muhimu.
Waziri Aweso ameiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa kuhusu Maji na Maendeleo Endelevu uliofanyika jijini Dushanbe, nchini Tajikistan.
Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa serikali, mashirika ya kimataifa, taasisi za kifedha na wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili mustakabali wa rasilimali za maji duniani.
Katika hotuba yake mbele ya jumuiya ya kimataifa, Waziri Aweso aliwasilisha kwa ufasaha mafanikio na mipango ya Tanzania katika Sekta ya Maji, huku akitoa mwaliko maalum kwa wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya maji.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na kuboresha sera, sheria na mifumo ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Kwa mujibu wa Waziri Aweso, Tanzania imefikia hatua muhimu katika kusogeza huduma za maji karibu na wananchi, ambapo utekelezaji unaendelea katika vijiji 1,575 vilivyobaki kati ya vijiji 12,333 nchini.
Hata hivyo, ili kufanikisha lengo la upatikanaji wa huduma bora kwa wote, kuna umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya majisafi na majitaka, matumizi ya teknolojia za kisasa, utafutaji wa vyanzo mbadala vya fedha pamoja na kujenga uwezo wa wataalam wa sekta.
Sera na Dira Vinavyovutia Wawekezaji
Moja ya hoja zilizovutia wadau wa kimataifa ni maboresho yaliyofanyika katika Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 Toleo la 2025 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Nyaraka hizi zimepanua fursa za ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya maji nchini.
Hatua hiyo inaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye mazingira rafiki kwa wawekezaji wanaotaka kushiriki katika miradi ya uzalishaji, uhifadhi, usambazaji na usimamizi wa rasilimali za maji.
Wadau wa maendeleo wanaeleza kuwa Sekta ya Maji imekuwa moja ya maeneo yenye mvuto mkubwa wa uwekezaji duniani kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo.
Kwa Tanzania, uwekezaji huo unaweza kusaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo mabwawa ya kuhifadhi maji, miradi ya maji vijijini pamoja na Gridi ya Taifa ya Maji inayotarajiwa kubadili sura ya upatikanaji wa huduma za maji nchini.
Ushirikiano wa Kimataifa Kufungua Milango ya Fursa
Mbali na kuhutubia mkutano huo, Waziri Aweso alifanya mazungumzo ya ngazi mbalimbali na viongozi wa kimataifa kwa lengo la kutafuta ushirikiano wa kiufundi na kifedha.
Miongoni mwa viongozi aliokutana nao ni Naibu Waziri Mkuu wa Tajikistan,Ziyozoda Sulaymon. Mazungumzo yao yalijikita katika namna Tanzania na Tajikistan zinavyoweza kushirikiana katika Sekta ya Maji, hususan katika uwekezaji wa miradi ya maji, matumizi ya teknolojia za kisasa na ujenzi wa mabwawa makubwa ya kuhifadhi maji.
Tajikistan ni miongoni mwa nchi zinazotambulika duniani kwa uzoefu wake katika usimamizi wa rasilimali za maji. Ushirikiano huo unatarajiwa kuipa Tanzania fursa ya kunufaika na utaalamu wa kimataifa katika kuendeleza sekta hiyo.
Aidha, Waziri Aweso alifanya mazungumzo ya kimkakati na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya Uchumi na Jamii, Li Junhua.
Katika kikao hicho, Tanzania iliwasilisha mahitaji yake ya ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maji pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuwa tishio kubwa kwa rasilimali za maji duniani kutokana na ukame, mafuriko na mabadiliko ya mifumo ya mvua.
Hivyo, ushirikiano na taasisi za Umoja wa Mataifa unachukuliwa kuwa hatua muhimu katika kuhakikisha Tanzania inapata msaada wa kitaalamu na kifedha kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hizo.
Gridi ya Taifa ya Maji na Fursa za Wawekezaji
Miongoni mwa miradi iliyowasilishwa kwa wadau wa kimataifa ni mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji. Mradi huu unalenga kuunganisha vyanzo vikuu vya maji na maeneo yenye mahitaji makubwa ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma za maji nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Aweso, utekelezaji wa mradi huo unahitaji uwekezaji mkubwa wa miundombinu, teknolojia na utaalamu wa hali ya juu. Hali hiyo inaifanya kuwa moja ya maeneo yenye fursa kubwa kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Kupitia mikutano aliyofanya na viongozi wa Tajikistan pamoja na taasisi za Umoja wa Mataifa, Tanzania imeanza kujenga msingi wa ushirikiano utakaosaidia kuvutia mitaji mipya, teknolojia za kisasa na maarifa muhimu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Mustakabali wa Sekta ya Maji Tanzania
Hatua za Waziri Aweso katika kutumia majukwaa ya kimataifa kutangaza fursa za uwekezaji zinaonesha mwelekeo mpya wa diplomasia ya maendeleo unaolenga kutafuta rasilimali na ushirikiano wa kimataifa kwa manufaa ya wananchi.
Kadri Tanzania inavyoendelea kutekeleza ajenda yake ya maendeleo ya mwaka 2050, Sekta ya Maji itaendelea kuwa mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda, kilimo, afya na ustawi wa jamii.
Kupitia mikakati ya kuvutia wawekezaji, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuendeleza matumizi ya teknolojia, Tanzania ina nafasi kubwa ya kufikia malengo yake ya kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora ya majisafi na salama.
Kwa hakika, juhudi za Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (Mb) katika kuitangaza Tanzania kwenye majukwaa ya kimataifa si tu zinatafuta uwekezaji wa leo, bali zinajenga msingi wa usalama wa maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa uchache hapa Tanzania Sekta ya Maji imenuia kuhakikiasha matumizi sawia ya maji na usimamizi endelevu wa rasilimali za maji kwa ajili ya kutokomeza umasikini, kuinua maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kuimarisha utangamano wa kikanda pamoja na ulinzi wa mazingira.
