Mjukuu wa Rais Museveni ambaye ni mtoto wa Jenerali Muhoozi Kainerugaba ahitimu mafunzo ya kijeshi Uingereza

NA DIRAMAKINI

RUHAMYA Kainerugaba ambaye ni Mjukuu wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na mtoto wa
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba amehitimu mafunzo ya uafisa katika Chuo cha Kijeshi cha Royal Military Academy Sandhurst nchini Uingereza, baada ya kukamilisha kozi ya wiki 44 ya kuwaandaa maafisa wa kijeshi.
Ruhamya alihitimu Ijumaa katika hafla iliyofanyika kwenye kampasi ya kihistoria ya chuo hicho mjini Camberley, Surrey pamoja na Kadeti mwingine kutoka Uganda, Andrew Bakira, na makadeti kutoka Uingereza na mataifa mengine washirika.

Hafla hiyo pia ilikuwa ya kipekee kwa familia ya Kainerugaba, baada ya Jenerali Muhoozi kuhudhuria sherehe hizo na kushuhudia mtoto wake akipokea kamisheni ya uafisa katika chuo kilekile alichohitimu miaka 26 iliyopita.

Jenerali Muhoozi alipokelewa na Kamanda wa Chuo cha Sandhurst, Meja Jenerali Nick Cowley OBE ambaye alimkabidhi medali maalumu ya wahitimu wa Sandhurst.

Medali hiyo ilianzishwa baada ya Jenerali Muhoozi kuhitimu chuo hicho mwaka 2000, na hivyo tukio la Ijumaa kuwa ishara ya mwendelezo wa kizazi hadi kizazi katika taaluma ya kijeshi.

MWANA NA BABA,MIAKA 27 YA TOFAUTI

Kabla ya hafla hiyo, Jenerali Muhoozi alishiriki picha zake akiwa kadeti pamoja na picha za mwanaye Ruhamya akiwa katika mafunzo, akieleza kuwa baba na mtoto walipitia changamoto zinazofanana za mafunzo, licha ya kutenganishwa na tofauti ya miaka 27.

Ujumbe huo uliweka bayana namna mafunzo ya Sandhurst yalivyokuwa sehemu ya safari ya kijeshi ya vizazi viwili vya familia hiyo.

MAFUNZO MAKALI YA UONGOZI WA KIJESHI

Kozi ya uafisa katika Chuo cha Royal Military Academy Sandhurst inatajwa kuwa miongoni mwa programu zenye mahitaji makubwa ya mafunzo ya uongozi wa kijeshi.

Katika kipindi cha wiki 44, makadeti hupitia mafunzo ya mbinu za kijeshi, matumizi ya silaha, ujuzi wa operesheni za uwanjani, mipango ya operesheni, maadili ya kijeshi pamoja na namna ya kufanya maamuzi na kuongoza wanajeshi katika mazingira yenye shinikizo.

Baada ya kuhitimu na kupewa kamisheni, Ruhamya na Bakira wanatarajiwa kurejea katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) kwa ajili ya kuendelea na majukumu ya kijeshi.
'SERVE TO LEAD’

Akizungumza na maafisa hao wapya, Mkuu wa Majeshi ya Nchi Kavu ya Uingereza, Jenerali Sir Roly Walker aliwaonya kuhusu mabadiliko yanayoendelea katika mazingira ya usalama duniani.

Alisema kipindi ambacho nchi za Magharibi zilikuwa na uhakika wa kutawala kijeshi duniani kinaelekea ukingoni, akibainisha kuwa mazingira ya kiusalama duniani yanazidi kuwa magumu na yasiyotabirika.

Kwa mujibu wa Jenerali Walker, mabadiliko hayo yanaongeza umuhimu wa kuwa na maafisa vijana wenye uwezo wa kuongoza wanajeshi na kuhakikisha majeshi yao yako tayari kukabiliana na changamoto za usalama.

Aliwakumbusha maafisa hao kuwa wajibu wao wa kwanza ni kujenga na kudumisha imani ya wanajeshi wanaowaongoza.

Akirejea kauli mbiu ya Chuo cha Sandhurst, “Serve to Lead”, Jenerali Walker alisema uongozi bora wa kijeshi unatokana na utayari wa kulitumikia taifa na kuwa mfano kwa wale wanaoongozwa.

Alisema,mataifa yatahitaji wanajeshi walio tayari kutekeleza majukumu yao, huku wanajeshi hao wakihitaji viongozi bora wenye uwezo wa kuwaongoza katika mazingira magumu.

Akihitimisha hotuba yake, alisema ana imani na kizazi kipya cha maafisa wa kijeshi, akisisitiza kuwa mustakabali wa majeshi uko mikononi mwa viongozi hao wapya.

UHUSIANO WA KIJESHI UGANDA NA UINGEREZA

Kuhitimu kwa maafisa wawili kutoka Uganda katika Chuo cha Sandhurst kunatajwa kuonesha kuendelea kwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Uganda na Uingereza.

Aidha, tukio hilo linaonesha jitihada za UPDF kuendelea kuwajengea uwezo maafisa wake kupitia mafunzo ya kijeshi katika taasisi za kimataifa, kwa lengo la kuimarisha taaluma, uongozi na weledi katika jeshi hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here