DAR-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt. Ngwaru Maghembe (Mb.), amekutana na Balozi wa Ethiopia nchini Tanzania, Mhe. Fekadu Beyene Ayana, anayemaliza muda wake wa uwakilishi nchini kwa ajili ya kumuaga.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Dkt. Maghembe amempongeza Balozi Ayana kwa mchango wake katika kuimarisha na kukuza uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia.
Ameeleza kuwa, katika kipindi cha uwakilishi wake, Balozi Ayana amekuwa sehemu muhimu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili, ikiwemo kufanikisha Mkutano wa Kwanza wa Pamoja wa Mawaziri kati ya Tanzania na Ethiopia, uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia mwezi Desemba 2024.
Mhe. Dkt. Maghembe amesema Wizara inaendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo, huku ikiendelea na maandalizi ya Mkutano wa Pili wa Pamoja wa Mawaziri unaotarajiwa kufanyika nchini Tanzania.
Aidha, Mhe. Dkt. Maghembe amemtakia Balozi Ayana kila la kheri na mafanikio katika majukumu yake yajayo, akimshukuru kwa ushirikiano alioutoa katika kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Balozi Ayana ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na mazingira mazuri aliyoyapata katika kipindi chake cha uwakilishi nchini.
Balozi huyo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia katika maeneo mbalimbali ya kimkakati, hususan kilimo, uchukuzi, nishati, miundombinu, viwanda na biashara.
Vilevile, ametumia fursa hiyo kueleza mipango ya Ubalozi wa Ethiopia nchini Tanzania, ikiwemo kuendeleza kiwanja cha Ubalozi kilichopo katika Mji wa Serikali, Mtumba, Dodoma.








