NA DIRAMAKINI
JUMUIYA ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imetoa wito wa amani,uvumilivu na ushiriki kamili wa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Zambia unaotarajiwa kufanyika kesho Agosti 13,2026.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Asasi ya Ushirikiano wa Siasa,Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC TROIKA) ambaye pia ni Rais wa Malawi, Profesa Arthur Peter Mutharika kupitia taarifa iliyotolewa leo Agosti 12, 2026.
Profesa Mutharika amesema, uchaguzi huo ni uchaguzi mkuu pekee uliopangwa kufanyika katika eneo la SADC mwaka huu, hivyo akasisitiza umuhimu wa mchakato huo kufanyika kwa amani na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.
Amesema,wananchi wa Zambia wanatarajiwa kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wao katika uchaguzi huo wa Agosti 13, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nchi nyingi wanachama wa SADC zimeonesha mshikamano kwa kutuma idadi kubwa ya waangalizi wa uchaguzi watakaoshiriki katika Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa SADC (SEOM).
Profesa Mutharika amesema, SEOM ina jukumu muhimu katika kuimarisha demokrasia kupitia uchaguzi wa mara kwa mara unaoaminika, huru, wa haki na wenye uwazi.
Ameeleza kuwa, ujumbe huo unatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Kanuni na Miongozo ya SADC ya Uchaguzi wa Kidemokrasia, ambayo inasisitiza umuhimu wa ushiriki jumuishi wa wananchi katika michakato ya uchaguzi.
Mwenyekiti huyo amewataka wananchi wote wenye sifa za kupiga kura nchini Zambia kutumia fursa hiyo kushiriki katika kuamua uongozi wa nchi yao kwa njia ya amani.
Amesisitiza kuwa,amani na uvumilivu vinapaswa kupewa kipaumbele si wakati wa kupiga kura pekee, bali pia katika kipindi chote baada ya uchaguzi.
“Ujumbe wangu leo ni kusisitiza umuhimu wa kuheshimu kwa kiwango cha juu amani na uvumilivu, wakati wa siku ya uchaguzi na baada yake,”amesema Profesa Mutharika.
SADC imeeleza kuwa,uchaguzi huo wa Zambia unatarajiwa kuwa na umuhimu katika kuendeleza mazingira ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yenye utulivu katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Jumuiya hiyo imesisitiza kuwa,ushiriki wa wananchi, kuheshimu taratibu za uchaguzi na kudumisha amani ni mambo muhimu katika kuhakikisha mchakato wa kidemokrasia unaleta matokeo yanayokubalika na kuchangia ustawi wa Zambia pamoja na ukanda mzima wa SADC.
