Serikali yasitisha leseni ya Gazeti la Mwanahalisi kwa kipindi cha miezi sita

NA DIRAMAKINI

IDARA ya Huduma za Habari (MAELEZO) imesitisha leseni ya uchapishaji wa gazeti la MwanaHALISI kwa kipindi cha miezi sita kuanzia leo Agosti 19, 2026 kwa madai ya kukiuka masharti ya leseni na kutofuata matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, pamoja na kanuni zake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara hiyo, gazeti hilo linadaiwa kukiuka Sharti la Tatu la Leseni ya Machapisho linalowataka watoa huduma za habari kuzingatia Sheria ya Huduma za Habari na Kanuni zake za mwaka 2017.

MAELEZO imeeleza kuwa l,ukiukaji huo ulitokana na habari iliyochapishwa katika kurasa za kwanza, pili na tatu za toleo namba 571 la gazeti hilo, lililochapishwa kati ya Agosti 6 na 12, 2026, chini ya kichwa cha habari, “Nchimbi agoma kujiuzulu.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, gazeti hilo lilichapisha habari hiyo bila kutimiza ipasavyo wajibu wa kuzingatia misingi ya usahihi na mizania ya habari kabla ya kuichapisha na kuisambaza kwa umma.

MAELEZO pia imesema uamuzi huo umezingatia kile ilichokiita mwenendo wa gazeti hilo wa kurudia makosa ambayo tayari liliwahi kuonywa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, MwanaHALISI lilipewa onyo la maandishi Mei 8, 2026, baada ya kubainika kwa makosa yaliyohusishwa na toleo namba 557, lililochapishwa Aprili 30 hadi Mei 6, 2026.

Idara hiyo imesisitiza kuwa,taaluma ya uandishi wa habari ni taaluma inayohitaji umakini na uangalifu mkubwa ili kuzuia upotoshaji na kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi na za kweli.

Aidha, imesema habari zinapaswa kutafutwa, kuchakatwa na kuchapishwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, weledi na misingi ya taaluma ya uandishi wa habari inayotambulika kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya Mkurugenzi wa Huduma za Habari (MAELEZO) kubaini madai ya ukiukaji wa masharti ya leseni yaliyowekwa chini ya Sheria ya Huduma za Habari, gazeti hilo lilipewa fursa ya kufika mbele ya Idara hiyo kwa ajili ya kusikilizwa kuhusu makosa yaliyodaiwa kufanyika.

Kikao hicho kilifanyika katika ofisi ndogo za MAELEZO jijini Dar es Salaam, Agosti 7, 2026.

Baada ya majadiliano, gazeti hilo lilipewa muda wa siku tatu kuwasilisha maelezo yake kwa maandishi kuhusu mazingira yaliyopelekea makosa hayo kutokea, kwa lengo la kumwezesha Mkurugenzi wa Huduma za Habari kuelewa kwa kina sababu na mazingira ya tukio hilo.




Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here