Soko bubu la madini lagundulika Dar,watuhumiwa 14 wakamatwa

NA DIRAMAKINI

SERIKALI imegundua soko bubu la madini jijini Dar es Salaam kupitia operesheni inayolenga kudhibiti biashara haramu ya madini, kuzuia utoroshaji wa madini na kuhakikisha mapato ya Serikali yanapatikana kupitia mfumo rasmi wa masoko ya madini nchini.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema zaidi ya watuhumiwa 14 wamekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya utoroshaji wa madini na wanatarajiwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria baada ya kukamilika kwa taratibu za uchunguzi.

Mavunde ameyasema hayo leo Agosti 9,2026, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini na kudhibiti mianya ya biashara isiyo rasmi.

Amesema,baadhi ya watu wamekuwa wakitumia nyumba za kupanga kama maeneo ya kufanya biashara ya madini kinyume na sheria, licha ya Serikali kuweka masoko na vituo vya ununuzi wa madini katika maeneo mbalimbali nchini.

“Hawa wenzetu, pamoja na Serikali kuwezesha masoko na vituo vya ununuzi vilivyosambaa nchi nzima, wao wameona waje kupanga nyumba na kuigeuza soko la madini,ambapo ni kinyume na sheria,”amesema.
Waziri Mavunde amesema, matumizi ya nyumba za kawaida kama vituo vya biashara ya madini yanaweza kuleta mianya ya utoroshaji wa madini na kuikosesha Serikali mapato yanayotokana na biashara hiyo.

Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa wamiliki wa nyumba kuhakikisha wanafahamu shughuli zinazofanywa na wapangaji wao ili kuepuka kuhusishwa na vitendo vinavyokiuka sheria.

“Natoa rai kwa wenye nyumba wote kuhakikisha wanafahamu shughuli za msingi za wapangaji wao ili kutojiingiza kwenye matatizo haya,”amesema.

UKAGUZI MAALUM KUANZA

Waziri huyo ametangaza kuwa, Serikali itafanya ukaguzi maalum katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam pamoja na mikoa mingine kwa lengo la kubaini nyumba na maeneo yanayotumika kama masoko yasiyo rasmi ya madini.
Amesema,hatua hiyo inalenga kuvunja mtandao wa biashara haramu ya madini na kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kupitia mifumo iliyowekwa kisheria.

“Tutafanya ukaguzi maalum kwenye baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine kubaini hizi nyumba zinazotumika kama soko la madini na kuwa chanzo cha utoroshaji madini,”amesema.

Aidha, Mavunde amesema taarifa za awali zinaonesha kuwa raia mmoja wa kigeni anahusishwa na shughuli hizo, akituhumiwa kuwezesha utoroshaji wa madini nje ya mfumo rasmi, na tayari amedhibitiwa na mamlaka.

Amevielekeza pia vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini na kuwakamata watu wote wanaohusika katika mnyororo wa biashara hiyo haramu, hatua inayolenga kuhakikisha kila anayehusika anawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

MADINI,VIFAA NA FEDHA VYAKAMATWA

Katika operesheni hiyo, Serikali imekamata jumla ya gramu 174 za madini, pamoja na vifaa mbalimbali vinavyodaiwa kutumika katika shughuli za uchambuzi na uchakataji wa dhahabu.

Vifaa vilivyokamatwa ni pamoja na mashine mbili za XRF aina ya NITON DXL 800, mizani ya kupimia uzito, mitungi ya gesi, vyungu vya kuchomea dhahabu, borax, vifaa vya gesi pamoja na vifaa vya kutengenezea maumbo ya dhahabu.

Mbali na madini na vifaa hivyo, Serikali pia imekamata Shilingi milioni 54,705,000 taslimu, ambazo ni miongoni mwa vitu vinavyoshikiliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Hatua hiyo inaashiria kuendelea kwa msako wa Serikali dhidi ya biashara ya madini inayofanyika nje ya mfumo rasmi, huku mamlaka zikilenga kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini yanauzwa na kusafirishwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa wafanyabiashara wa madini kutumia masoko na vituo rasmi vya ununuzi vilivyowekwa nchini, hatua inayosaidia kuimarisha uwazi katika biashara ya madini, kulinda maslahi ya wachimbaji na kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki.

Aidha,operesheni hiyo pia inaweka mkazo katika ushirikiano kati ya Wizara ya Madini, vyombo vya dola na wadau wengine katika kukabiliana na mitandao inayoweza kujihusisha na utoroshaji wa madini na biashara isiyo rasmi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here