NA DIRAMAKINI
MKOA wa Iringa unaendelea kujivunia urithi muhimu wa kihistoria kupitia Makumbusho ya Mtwa Mkwawa yaliyopo katika Kijiji cha Kalenga, Kata ya Kalenga Wilaya ya Iringa Vijijini, takribani kilomita 12 kutoka Manispaa ya Iringa.
Makumbusho hiyo inayosimamiwa na Makumbusho ya Taifa la Tanzania, imeendelea kuwa kivutio muhimu kwa watalii wa ndani na nje ya nchi wanaofika kujifunza historia ya jamii ya Wahehe na kumuenzi aliyekuwa Chifu wa Wahehe, Mkwawa ambaye alijulikana kwa msimamo wake wa kupinga utawala wa kikoloni.
Mhifadhi wa Mambo ya Kale katika Makumbusho ya Mtwa Mkwawa, Bi.Zuhura Mohamed amesema, eneo hilo lina umuhimu mkubwa katika kuhifadhi historia, utamaduni na kumbukumbu za jamii ya Wahehe, huku likitoa fursa kwa vizazi vya sasa na vijavyo kujifunza historia kwa vitendo.
Bi.Mohamed amesema, Makumbusho ya Mtwa Mkwawa si eneo la kutazama tu vitu vya kale, bali ni sehemu muhimu ya urithi wa taifa inayobeba kumbukumbu za maisha, utamaduni na mapambano ya jamii ya Wahehe katika vipindi mbalimbali vya historia.
Miongoni mwa vivutio vikuu vinavyowavutia wageni katika eneo hilo ni fuvu linalotambuliwa kuwa la Chifu Mkwawa, mmoja wa viongozi mashuhuri wa Wahehe katika historia ya Tanzania.
Chifu Mkwawa anakumbukwa kwa mapambano dhidi ya uvamizi wa Wajerumani katika eneo la Tanganyika wakati wa utawala wa kikoloni.
Historia yake na mapambano hayo vimeifanya Kalenga kuwa miongoni mwa maeneo muhimu yanayotembelewa na watu wanaotaka kufahamu historia ya upinzani dhidi ya ukoloni.
Mbali na fuvu hilo, wageni wanaotembelea Makumbusho ya Mtwa Mkwawa hupata fursa ya kuona mabaki ya Ngome ya Lipuli, ambayo inatajwa kuwa sehemu ya ngome zilizohusishwa na ulinzi wa maeneo yaliyokuwa chini ya Chifu Mkwawa.
Ngome hiyo ni sehemu ya urithi unaosaidia kueleza namna jamii ya Wahehe ilivyokuwa ikiandaa mifumo yake ya ulinzi na kukabiliana na changamoto za kiusalama katika kipindi hicho.
Eneo la Makumbusho ya Mtwa Mkwawa pia linahifadhi makaburi ya baadhi ya machifu pamoja na majengo ya kihistoria yanayotoa picha ya maisha ya jamii na mabadiliko yaliyotokea katika eneo hilo wakati wa utawala wa kikoloni.
Aidha, kuna maeneo yenye miti iliyokuwa ikitumika katika shughuli za ibada na mila za mababu, hali inayolifanya eneo hilo kuwa muhimu katika kuhifadhi historia na utamaduni wa jamii za eneo hilo.
Silaha za jadi pamoja na baadhi ya silaha zilizotumika katika kipindi cha mapambano dhidi ya Wajerumani, hususan katika maeneo yaliyohusishwa na vita vya Lugalo, pia ni sehemu ya urithi unaowekwa katika mazingira ya makumbusho hayo.
Kituo cha elimu ya historia.
Makumbusho hiyo imekuwa pia kituo cha kujifunzia historia kwa wanafunzi na wageni wa rika mbalimbali.
Wanafunzi kutoka shule na taasisi mbalimbali za elimu hupata fursa ya kutembelea eneo hilo na kujifunza historia kwa vitendo, jambo linalosaidia kuongeza uelewa kuhusu historia ya Tanzania, utamaduni wa Wahehe na mchango wa maeneo ya kihistoria katika kujenga kizazi kinachothamini urithi wa taifa.
Bi.Mohamed amewataka wananchi, hususan Watanzania kutumia fursa hiyo kutembelea Kalenga ili kujifunza na kuenzi historia ya taifa.
Kwa mujibu wa Mhifadhi huyo, viingilio katika makumbusho hayo vimepangwa kwa kuzingatia makundi mbalimbali ya wageni.
Amesema, kwa wakazi wa Afrika Mashariki, watu wenye umri wa miaka 17 na kuendelea hulipa Shilingi 2,360, huku watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 16 wakitozwa Shilingi 1,180.
Kwa wageni kutoka nje ya Afrika Mashariki, kiingilio kwa watu wazima ni Dola za Marekani 10, wakati watoto hulipa Dola tano.
Aidha, wageni wenye vibali maalum hulipa Dola za Marekani tano kwa watu wazima na Dola 2.5 kwa watoto.
Uongozi wa Makumbusho ya Mtwa Mkwawa umesisitiza umuhimu wa wananchi kutembelea maeneo ya kihistoria kama Kalenga kwa lengo la kujifunza, kutafakari na kuendeleza utamaduni wa kutembelea vivutio vya ndani.
Ujumbe unaobebwa na historia ya Kalenga ni pamoja na ujasiri, uzalendo na mshikamano wa jamii katika kulinda ardhi na maslahi yake.
Kupitia ziara za wanafunzi na wageni wengine, historia hiyo inaendelea kuwasilishwa kwa vizazi vipya ili kuwafanya watambue mchango wa waliowatangulia na umuhimu wa kuhifadhi urithi wa taifa.
“Utalii unaanza na sisi.” ni miongoni mwa kaulimbiu inayosisitizwa na uongozi wa makumbusho hiyo, ikiwa ni wito kwa Watanzania kutembelea Kalenga, kujifunza historia na kuenzi urithi wa mashujaa wa taifa.














