DAR-Serikali imeitaka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) kuharakisha maboresho ya mitaala na mafunzo ya uhasibu ili kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya akili unde (AI), kwa kuwa baadhi ya kazi zinazofanywa na wahasibu hivi sasa zinaweza kubadilika au kutoweka kutokana na mapinduzi hayo ya kiteknolojia.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), wakati akihutubia kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 49 ya NBAA yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha APC-Mbweni, jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Luswetula amesema, dunia inaelekea kwa kasi katika matumizi ya akili unde na kwamba taaluma ya uhasibu haiwezi kubaki nyuma katika mabadiliko hayo, kwa kuwa inaleta mabadiliko katika namna kazi mbalimbali zinavyofanyika na kwamba ni muhimu wataalamu wa uhasibu kuandaliwa mapema ili waweze kutumia teknolojia hiyo kuongeza ufanisi na tija badala ya kuachwa nyuma na mabadiliko ya kiteknolojia.
"Dunia yote inaelekea kwenye matumizi ya akili unde, na NBAA pamoja na wadau wengine muangalie mmejipangaje kukabiliana na mapinduzi haya hasa kuhakikisha mitaala yetu ya mafunzo imesharekebishwa ili kuendana na mwelekeo wa dunia ya sasa,”amesema Mhe. Luswetula.Amesisitiza kuwa, Kama Taifa kuna umuhimu wa kuongeza idadi ya wataalamu wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini kwa kuzingatia suala la ubora, weledi, uaminifu na uadilifu kama msingi wa taaluma hiyo, kwa kuwa idadi ya wahasibu wenye sifa bado haitoshelezi mahitaji yaliyopo katika sekta ya umma na binafsi.
Mhe. Luswetula amesema kuwa, wahasibu na wakaguzi wa hesabu wana nafasi muhimu katika kulinda na kusimamia rasilimali za Taifa, kwa kuwa taaluma hizo ni miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi, hivyo wataalamu wake wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia viwango vya juu vya uadilifu na uaminifu.
"Naitaka NBAA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta suluhisho la changamoto ya ukosefu wa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa uhasibu, kwa sababu wahitimu wengi wanapata elimu ya nadharia darasani zaidi lakini wanakutana na changamoto wanapoingia katika mazingira halisi ya kazi kutokana na kukosa fursa za kutosha za kujifunza kwa vitendo,” amesema Mhe. Luswetula.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na NBAA, ikiwemo kuhakikisha Bodi hiyo inakuwa na watumishi wa kutosha na wenye weledi unaohitajika huku akiwapongeza wahitimu wa programu mbalimbali za NBAA, ikiwemo Taaluma ya Juu ya Uhasibu (CPA), Cheti cha Uhasibu (ATEC), CPA Equivalent, Stashahada ya Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (IPSAS), Stashahada ya Kitaalamu katika Ukaguzi wa Ndani (Professional Diploma in Internal Auditing) na Stashahada ya Kitaalamu katika Utoaji wa Taarifa za Uendelevu (Professional Diploma in Sustainability Reporting).




