Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato wafikia asilimia 89

NA DIRAMAKINI

UJENZI wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma umeingia katika hatua ya mwisho, huku kazi za miundombinu zikifikia asilimia 89 na ujenzi wa majengo ukifikia asilimia 78.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta amesema, kazi za miundombinu zinatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu, wakati zile za majengo zikitarajiwa kukamilika Desemba.

Mhandisi Besta amesema,TANROADS inaendelea kufuatilia kwa karibu ratiba za utekelezaji za wakandarasi, upatikanaji na ufungaji wa vifaa pamoja na uratibu wa shughuli zinazotegemeana ili kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati.

Mradi huo unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ukiwa na lengo la kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga nchini na kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria na mizigo.

Aidha, uwanja huo unatarajiwa kuipa Dodoma uwanja wa ndege wa kisasa wa kimataifa utakaowezesha huduma za ndege za ndani na nje ya nchi, huku ukifungua fursa zaidi za biashara, uwekezaji, utalii, usafirishaji wa mizigo na ajira.

Kwa mujibu wa Mhandisi Besta, awamu ya kwanza ya mradi huo inatekelezwa kupitia hatua mbili zinazohusisha ujenzi wa miundombinu na majengo.

Amesema hadi sasa, hatua ya kwanza imefikia asilimia 89.02 ya utekelezaji, ambapo ujenzi wa njia kuu ya ndege (runway) ulikuwa umefikia asilimia 98, huku njia za kuingia na kutoka kwa ndege (taxiways) pamoja na eneo la maegesho ya ndege (aircraft apron) kila moja likiwa limefikia asilimia 99.

Amesema, ujenzi wa barabara za kuingia na za ndani ya uwanja pamoja na maeneo ya maegesho ya magari umefikia asilimia 75, huku mfumo wa upatikanaji wa maji ukiwa umefikia asilimia 89.

Kwa upande mwingine, ujenzi wa uzio na mageti umefikia asilimia 76, wakati kazi za umeme pamoja na vifaa vya kuongozea ndege zimefikia asilimia 90.

Mhandisi Besta amesema, kazi zilizobaki katika hatua hiyo ni pamoja na uwekaji wa mandhari na upandaji nyasi katika maeneo ya usalama, ufungaji wa taa za uwanja na barabara, uwekaji wa mabomba ya maji na tenki la maji la chini ya ardhi, ukamilishaji wa uzio pamoja na ufungaji wa mifumo ya mawasiliano na urambazaji wa ndege.

Kuhusu majengo amesema,utekelezaji wake umefikia asilimia 78.37, ambapo jengo la abiria limefikia asilimia 81, mnara wa kuongozea ndege asilimia 74, kituo cha zimamoto asilimia 88 na jengo la huduma za hali ya hewa asilimia 87.

Aidha, amesema mradi huo umewezesha ajira kwa Watanzania 9,059, ambapo 3,571 wameajiriwa katika hatua ya kwanza na 5,488 katika hatua ya pili. Wafanyakazi 47 kutoka nje ya nchi nao wamehusishwa katika utekelezaji wa mradi huo.

Uwanja huo unajengwa kwa kuzingatia viwango vya Category 4E vya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), ukiwa na njia kuu ya ndege yenye urefu wa mita 3,600.

Aidha,unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia hadi abiria milioni 1.5 kwa mwaka na kupokea ndege kubwa ikiwemo Boeing 787 Dreamliner.

Mhandisi Besta amewataka wakazi wa Dodoma kujiandaa kutumia fursa za kiuchumi na kibiashara zinazotarajiwa kujitokeza baada ya uwanja huo kuanza kufanya kazi, akisema mradi huo utakuwa kichocheo cha shughuli mbalimbali za maendeleo katika mji huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here