NA DIRAMAKINI
MAMLAKA nchini Zimbabwe zimethibitisha kutokea kwa ajali mbaya ya helikopta katika eneo la Marondera, mashariki mwa mji mkuu Harare, iliyosababisha vifo vya watu wote waliokuwa ndani.
Kwa mujibu wa Polisi wa Jamhuri ya Zimbabwe (ZRP), ajali hiyo imetokea Jumatano jioni Septemba 30, 2026 majira ya saa 11 jioni (5pm) katika eneo la Marondera Vijijini, Mkoa wa Mashonaland East.
Msemaji wa Polisi, Kamishna Paul Nyathi, amesema,helikopta hiyo ilikuwa na watu sita ndani.Miili ya marehemu iliteketea vibaya na itahitaji utambuzi rasmi.
Msemaji wa Serikali ya Zimbabwe, Nick Mangwana, amethibitisha kupitia taarifa: "Taarifa za sasa zinaonesha hakuna aliyenusurika katika ajali hii."
Tajiri maarufu Wicknell Chivayo na mkewe Lucy "Lulu" Muteke wametajwa kuwa miongoni mwa waliofariki.
Kifo chake kimethibitishwa na msemaji wa familia, Herbert Chivayo, aliyeliambia shirika la habari la taifa ZBC kuwa,familia ina majonzi makubwa kufuatia msiba huo.
Polisi wamesema, helikopta hiyo ilikuwa imebeba mfanyabiashara huyo, abiria wengine watatu na marubani wawili.
Uchunguzi wa kubaini chanzo cha ajali hiyo unaendelea na polisi wamesema, watatoa taarifa kamili hivi karibuni.(NA)
