NA GODFREY NNKO
SERIKALI ya Tanzania imepiga hatua nyingine katika sekta ya afya na teknolojia ya tiba, baada ya Hospitali ya Taifa ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma kuanza kutoa huduma ya kudhibiti maumivu wakati wa kujifungua kwa kutumia teknolojia ya Epidural Analgesia, inayomwezesha mama kujifungua akiwa na maumivu yaliyopunguzwa kwa kiwango kikubwa.
Huduma hiyo imeelezwa kuwa, hatua muhimu katika kuboresha uzoefu wa mama wakati wa kujifungua, kwa kupunguza maumivu makali yanayoambatana na uchungu wa uzazi, huku ikimuwezesha mama kubaki na fahamu, kushirikiana na wataalamu wa afya na kuendelea kuhisi uchungu pamoja na msukumo wa mtoto kushuka.
Akizungumza kupitia mahojiano maalumu na MAELEZO TV, Daktari Bingwa wa Usingizi na Ganzi Tiba kutoka Hospitali ya Taifa ya Benjamin Mkapa, Dkt. Lugano Wilson amesema, Epidural Analgesia hufanya kazi kwa kudhibiti usafirishaji wa taarifa za maumivu kutoka sehemu mbalimbali za mwili kwenda kwenye ubongo, bila kuzuia mchakato wa kawaida wa kujifungua.
Amesema, tofauti na dhana kwamba huduma hiyo humfanya mama asihisi kabisa kinachoendelea wakati wa kujifungua, Epidural Analgesia inalenga zaidi kupunguza au kudhibiti maumivu, huku hisia muhimu zinazomsaidia mama kushiriki katika mchakato wa uzazi zikiendelea kuwepo.
“Unapopata maumivu, ubongo unapokea taarifa kwamba kuna sehemu mwili unashughulika. Tunachofanya sisi ni kudhibiti taarifa hiyo isisafiri kwenda kwenye ubongo, lakini mchakato mzima wa uzazi, ikiwemo mama kusikia mikazo na msukumo wa mtoto kushuka, unabaki kama ulivyo,” amesema Dkt.Wilson.
Dkt.Wilson amesema, huduma hiyo huanza kutolewa baada ya uchungu wa uzazi kuanza rasmi na mlango wa kizazi kufunguka kwa takribani sentimita nne, hatua ambayo huashiria kuingia katika awamu muhimu ya leba.
Amesema,baada ya dawa kutolewa, huanza kufanya kazi ndani ya dakika 10 hadi 20, huku mama akiendelea kuwa na fahamu kamili na uwezo wa kushirikiana na wakunga katika hatua mbalimbali za kujifungua.
Mtaalamu huyo amesema, mama anaweza kuendelea kuhisi uchungu na msukumo wa mtoto kushuka, lakini maumivu makali hupunguzwa, hivyo kumpa nafasi ya kuendelea kushiriki katika mchakato wa kujifungua akiwa katika hali ya utulivu zaidi.
Pamoja na faida zake, wataalamu wa afya wameeleza kuwa, Epidural Analgesia si huduma inayotolewa kiholela kwa kila mama mjamzito, bali inahitaji tathmini ya kitaalamu kabla ya kuanza kutumika.
Hospitali ya Taifa ya Benjamin Mkapa imeanzisha kliniki maalumu inayowahudumia wajawazito kuanzia wiki ya 32 ya ujauzito, ambapo mama hupata elimu, ushauri na tathmini ya kitabibu ili kubaini kama anafaa kupata huduma hiyo.
Dkt.Wilson amesema, baadhi ya hali zinazoweza kumfanya mama ashauriwe kutotumia huduma hiyo ni pamoja na kuwa na changamoto za kuganda kwa damu, kuwa na maambukizi katika eneo ambalo sindano ya ganzi inapaswa kuchomwa, pamoja na baadhi ya hali za kitabibu zinazohitaji kujifungua kwa upasuaji moja kwa moja.
Hivyo, uamuzi wa kutumia Epidural Analgesia hufanywa baada ya wataalamu wa afya kumfanyia mama tathmini na kujiridhisha kuhusu usalama wake na wa mtoto.
Mbali na hayo, huduma hiyo inatajwa kuwa na manufaa kadhaa katika mchakato wa kujifungua, hasa kwa upande wa kudhibiti maumivu na kumsaidia mama kutoa ushirikiano wa kutosha wakati akiwa leba.
Huduma hiyo, inapunguza mzigo wa maumivu makali na msongo wa mawazo unaoweza kuambatana na uchungu wa muda mrefu.
Mosi, kwa mama anayepitia leba yenye maumivu makali, udhibiti wa maumivu unaweza kumsaidia kuwa mtulivu na kuelekeza nguvu zake katika kufuata maelekezo ya wataalamu.
Pili, kupungua kwa maumivu kunaweza kumwezesha mama kushirikiana vizuri zaidi na wakunga, hasa katika hatua ya kusukuma mtoto, badala ya kutumia nguvu nyingi kukabiliana na maumivu pekee.
Tatu, huduma hiyo inalenga kuboresha uzoefu wa mama katika kujifungua kwa kumpa mazingira yenye utulivu na faraja zaidi, huku usalama wa mama na mtoto ukiendelea kuwa jambo la msingi.
Ujio wa huduma hiyo pia umeibua mjadala kuhusu namna teknolojia ya tiba inavyoweza kubadili uzoefu wa wanawake katika uzazi.
Kwa muda mrefu, maumivu makali yamekuwa yakihusishwa na mchakato wa kawaida wa kujifungua, hali ambayo kwa baadhi ya wanawake imekuwa chanzo cha hofu kabla na wakati wa ujauzito.
Aidha, kwa kutumia mbinu za kisasa za udhibiti wa maumivu, wataalamu wa afya wanaweza sasa kumsaidia mama kukabiliana na leba bila kuondoa kabisa uwezo wake wa kutambua kinachoendelea katika mwili wake.
Dhana hiyo imekuwa ikitumika katika mifumo mbalimbali ya afya duniani, ikiwemo katika nchi zenye huduma zilizoendelea za uzazi, ambapo udhibiti wa maumivu wakati wa leba ni miongoni mwa huduma zinazopatikana kwa wanawake wanaokidhi vigezo vya kitabibu.
Akizungumzia mitazamo ya baadhi ya wananchi wanaohusisha huduma hiyo na imani za kidini au mila zinazotaja mwanamke kujifungua kwa uchungu, Dkt. Wilson amesema,maendeleo ya tiba hayalengi kupingana na imani, bali kutafuta namna ya kupunguza mateso na kuboresha afya ya binadamu.
Ametumia mfano wa maendeleo ya teknolojia katika shughuli za kila siku, akisema kama ambavyo jamii imekubali kutumia magari badala ya kutembea kwa miguu na matrekta badala ya kutegemea nguvu kazi pekee katika kilimo, ndivyo sayansi ya tiba inavyoendelea kutafuta njia za kukabiliana na changamoto za kiafya.
“Kama ambavyo tunapanda magari badala ya kutembea kwa miguu kwenda mashambani na kutumia matrekta kulima, ndivyo ambavyo teknolojia inazidi kurahisisha maisha na kutatua changamoto za kibinadamu,” amesema.
Tags
Afya
Epidural Analgesia
Habari
Hospitali ya Taifa ya Benjamin Mkapa (BMH)
Makala
Makala kwa Kina
Sayansi na Teknolojia
Tanzania
Teknolojia


