BRELA kuimarisha huduma za kielektroniki na ustawi wa watumishi wake

NA GODFREY NNKO

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umeweka kipaumbele katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa njia za kielektroniki, kuboresha mifumo ya usajili na leseni, pamoja na kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Hatua hizo zimebainishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw.Godfrey Nyaisa wakati akihitimisha kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa wakala huo kilichofanyika katika Hoteli ya Timeless mkoani Morogoro leo Oktoba 11, 2026, ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dennis Londo.

Bw.Nyaisa amesema kuwa, BRELA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali, mpango mkakati wa taasisi wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031, pamoja na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Amesema, maeneo yatakayopewa msukumo ni pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kupitia mifumo ya kielektroniki, kukamilisha maboresho ya mfumo wa BRELA Online Service (BOS), kuwezesha utoaji wa leseni za biashara za Kundi B kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Sambamba na kuendelea kupitia sheria na kanuni zinazohusu usajili na leseni ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Amesema, hatua hizo zinalenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kuboresha uzoefu wa wateja na kuhakikisha wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji wanapata huduma zinazokidhi mahitaji yao.

Bw.Nyaisa amesema kuwa, matumizi yenye tija ya rasilimali, usimamizi wa utendaji na uwajibikaji vitaendelea kupewa kipaumbele ili kuwezesha wakala kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Akizungumzia matokeo ya kikao hicho, Bw. Nyaisa amesema, Baraza la Wafanyakazi limekuwa jukwaa muhimu la kutathmini utekelezaji wa majukumu ya taasisi, kujadili changamoto zinazojitokeza kazini na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji pamoja na ustawi wa watumishi.

Amesema, katika kikao hicho, wajumbe walipokea na kujadili taarifa ya utendaji wa BRELA kwa mwaka wa fedha 2025/2026, taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya kikao kilichopita pamoja na hoja na changamoto mbalimbali zilizowasilishwa na watumishi.

Ameeleza kuwa, pia baraza lilipokea na kuridhia mafanikio yaliyopatikana katika maeneo ya usajili wa kampuni na majina ya biashara, usajili na ulinzi wa miliki bunifu, utoaji wa leseni za biashara na viwanda, pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Bw. Nyaisa amesema, mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara, Bodi ya Ushauri ya BRELA, menejimenti na watumishi wa wakala huo.

Hata hivyo, amebainisha kuwa, bado kuna maeneo yanayohitaji maboresho, hususan kuongeza kasi ya utoaji wa huduma, kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuboresha uzoefu wa wateja wanaohudumiwa na taasisi hiyo.

Amesema, menejimenti imepokea maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe wa baraza na itaendelea kuyafanyia kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo ya utumishi wa umma na upatikanaji wa rasilimali.

Maazimio kufuatiliwa hadi utekelezaji

Bw. Nyaisa ameahidi kuwa, maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho yatawekewa mpango wa utekelezaji utakaobainisha hatua zinazopaswa kuchukuliwa, wahusika na muda wa utekelezaji.

Amesema, menejimenti pia itaimarisha mifumo ya ufuatiliaji na utoaji wa mrejesho ili kuhakikisha maazimio hayo yanatekelezwa kwa wakati na kuleta maboresho yanayotarajiwa katika utendaji wa taasisi.

Pia, amesisitiza kuwa, mafanikio ya kikao cha baraza hayatapimwa kwa idadi ya hoja zilizojadiliwa pekee, bali kwa hatua zitakazochukuliwa kutekeleza maazimio na matokeo yatakayopatikana katika kuboresha huduma kwa wananchi na mazingira ya kazi ya watumishi.

Vilevile, amesema ushirikiano kati ya menejimenti, wafanyakazi na wadau wengine ni muhimu katika kuhakikisha BRELA inafikia malengo yake na kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.

Wakati huo huo, Nyaisa amesema, menejimenti inatambua kuwa, mafanikio ya taasisi yanategemea uwepo wa watumishi wenye ujuzi, weledi na motisha ya kutekeleza majukumu yao.

Amesema, kwa msingi huo, BRELA itaendelea kuwekeza katika kuendeleza uwezo wa watumishi, kuboresha mazingira ya kazi na kushughulikia masuala yanayohusu maslahi yao kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Aidha, amesema wakala huo unaendelea kuunga mkono juhudi za kuanzishwa kwa BRELA SACCOS Limited, ambayo inalenga kuwa sehemu ya mikakati ya kuimarisha ustawi wa kiuchumi wa watumishi.

Bw. Nyaisa ameeleza kuwa, ushirika huo unatarajiwa kuwa nyenzo ya kuhamasisha utamaduni wa kuweka akiba, kujenga uwezo wa kifedha na kuwawezesha watumishi kupata huduma za kifedha.
Bw. Nyaisa ametoa wito kwa watumishi kushiriki katika juhudi za kuimarisha ushirika huo ili uweze kuchangia katika kuboresha ustawi wao wa kiuchumi.

Amesema, menejimenti itaendelea kushirikiana na watumishi na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa hoja zinazowasilishwa katika vikao vya baraza zinapata ufumbuzi unaozingatia taratibu na mahitaji ya taasisi.

TUGHE yapongeza menejimenti ya BRELA

Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Mkuu Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) ambaye  ni Katibu wa TUGHE Mkoa wa Morogoro, Bw. Anthelmus Tarimo ameipongeza menejimenti ya BRELA kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake na kuwahudumia wananchi wanaohitaji huduma za usajili wa kampuni, taasisi na leseni.

Mwakilishi huyo amesema, TUGHE inatambua umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi kama chombo cha kuwakutanisha mwajiri na wafanyakazi ili kujadili masuala yanayohusu utendaji, maslahi ya watumishi na maendeleo ya taasisi.

Amesema, ushiriki wa chama hicho katika baraza unalenga kuhakikisha majadiliano na maamuzi yanazingatia taratibu, miongozo na makubaliano yaliyowekwa kati ya TUGHE na menejimenti ya BRELA.

Kwa mujibu wa mwakilishi huyo, chama hicho kinafurahishwa na ushirikiano unaoendelea kati ya menejimenti na wafanyakazi, hususan katika kushughulikia masuala ya motisha na kuboresha maslahi ya watumishi.

Amesema, huduma zinazotolewa na BRELA zina mchango muhimu katika kurahisisha usajili wa biashara na taasisi, hatua inayowezesha shughuli za kiuchumi kuanzishwa na kuendelezwa na hivyo kuchangia upatikanaji wa ajira kwa Watanzania.

Ameongeza kuwa, kampuni na taasisi zinazopata huduma za usajili na leseni zina nafasi ya kuchangia maendeleo ya uchumi na kuongeza fursa za ajira, jambo ambalo pia lina umuhimu kwa vyama vya wafanyakazi vinavyowakilisha maslahi ya waajiriwa.
Katibu wa TUGHE Mkoa wa Morogoro, Bw. Anthelmus Tarimo ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa katika mkutano huo.

Mwakilishi huyo amesema, TUGHE itaendelea kushirikiana na menejimenti ya BRELA katika kuibua mawazo chanya, kutoa ushauri na kuhamasisha utekelezaji wa mipango ya taasisi kwa manufaa ya mwajiri na wafanyakazi.

Amesisitiza kuwa, Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu la kuimarisha mawasiliano, kujadili changamoto na kutafuta suluhisho zinazoweza kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

Wakati huo huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Nyaisa ameishukuru Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwongozo na usimamizi wake, Bodi ya Ushauri ya BRELA kwa ushauri, pamoja na viongozi wa TUGHE, wajumbe wa baraza, wawezeshaji na sekretarieti kwa mchango wao katika kufanikisha kikao hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here