Naibu Waziri Londo aitaka BRELA kulinda biashara za Watanzania

NA GODFREY NNKO

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dennis Londo ameitaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuimarisha mifumo ya usajili na usimamizi wa biashara ili kulinda fursa za kiuchumi za Watanzania, kupunguza urasimu na kuweka mazingira bora kwa biashara na uwekezaji nchini.
Mheshimiwa Londo ametoa wito huo leo Oktoba 11, 2026 wakati akifunga kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa BRELA kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kilichofanyika katika Hoteli ya Timeless mkoani Morogoro.

Amesema, BRELA ina wajibu mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2020–2050, hasa katika kurasimisha biashara ndogo, za kati na kubwa, kukuza uwekezaji, kuongeza thamani ya bidhaa na kuwezesha Watanzania wengi zaidi kushiriki katika shughuli za uzalishaji na biashara.

Mheshimiwa Londo amesisitiza kuwa, juhudi za kuboresha mazingira ya biashara zinapaswa kwenda sambamba na hatua za kuhakikisha kuwa Watanzania wanalindwa dhidi ya vitendo vinavyoweza kuwanyima fursa za kushiriki katika shughuli za kiuchumi zinazopaswa kuwa ndani ya uwezo wao kwa mujibu wa sheria.

Aonya kuhusu matumizi ya majina ya Watanzania

Naibu Waziri huyo ameeleza wasiwasi wake kuhusu baadhi ya watu kutumia majina na vitambulisho vya Watanzania kufungua kampuni kwa niaba ya raia wa kigeni, kwa lengo la kukwepa masharti na taratibu zilizowekwa na Serikali katika kulinda fursa za kiuchumi na ajira za wananchi.

Ameitaka BRELA kutumia mifumo, utaalamu na uwezo wake wa kitaasisi kuchukua hatua zinazostahili, kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ili kuzuia vitendo hivyo na kuhakikisha sheria na taratibu za usajili wa kampuni zinafuatwa.

Pia, amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kuwa, Watanzania wanapata nafasi ya kushiriki katika biashara na uwekezaji, huku ikihakikisha kuwa shughuli hizo zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria za nchi.

Kwa mujibu wa Londo, jukumu hilo linahitaji ushirikiano wa karibu kati ya BRELA na taasisi nyingine za Serikali ili kubaini mianya inayoweza kutumiwa kukwepa masharti ya kisheria na kuimarisha ulinzi wa fursa za biashara kwa wananchi.

Amebainisha kuwa, urasimishaji wa biashara ni sehemu muhimu ya kujenga uchumi jumuishi, unaowezesha wananchi kushiriki katika maendeleo kupitia vipaji, ujuzi na shughuli zao za uzalishaji.

Apongeza maboresho ya huduma za kielektroniki

Wakati huo huo, Mheshimiwa Londo ameipongeza BRELA kwa mafanikio yaliyopatikana katika matumizi ya teknolojia, hususan maboresho ya mifumo ya usajili wa kampuni na huduma nyingine zinazotolewa kwa njia ya kielektroniki.

Amesema, taarifa ya utendaji wa wakala kwa mwaka wa fedha 2025/2026 imeonesha mafanikio katika utoaji wa huduma mbalimbali, huku baadhi ya malengo yaliyowekwa yakivukwa.

Ameeleza kuwa, mafanikio hayo yamechangiwa na juhudi za menejimenti na watumishi, pamoja na kuimarishwa kwa mifumo ya kielektroniki inayorahisisha utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Londo amesema, matumizi ya teknolojia yanapaswa kuendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa kusubiri huduma na kurahisisha shughuli za usajili kwa wananchi na wafanyabiashara.

Amesema, hatua ya BRELA kuanza kutumia moduli tano kati ya saba zilizopangwa katika maboresho ya huduma za mtandaoni ni maendeleo yanayopaswa kuendelezwa hadi mifumo yote iliyokusudiwa ikamilike.

Hata hivyo, Mheshimiwa Londo ameiagiza menejimenti kuhakikisha maboresho hayo yanakamilika kwa wakati huku mifumo ikiwa imara, salama na rahisi kutumiwa na wananchi.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kutatua changamoto zinazojitokeza katika mifumo hiyo kwa wakati ili kuhakikisha kuwa mabadiliko ya kiteknolojia yanaboresha huduma badala ya kuwa kikwazo kwa watumiaji.

Amesema, mafanikio ya taasisi hayawezi kupimwa kwa idadi ya huduma zinazotolewa pekee, bali pia kwa ubora wa huduma hizo na mchango wake katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Naibu Waziri huyo ameonya kuwa, taasisi hazipaswi kujipima kwa mafanikio yanayoonekana ndani pekee, bali zinapaswa kuzingatia maoni, malalamiko na matarajio ya wananchi wanaopokea huduma.

Amesema, taasisi inaweza kudai imevuka malengo yake, lakini ikiwa wananchi bado wanakabiliwa na changamoto zinazoweza kutatuliwa, bado kuna wajibu wa kuendelea kuboresha utendaji.

Mheshimiwa Londo amesema, BRELA inapaswa kuendelea kufanya mapitio ya sheria, kanuni na taratibu zinazohusiana na biashara na utoaji wa huduma, kwa kushirikiana na wadau husika, ili kuondoa vikwazo visivyo vya lazima na kuimarisha uzingatiaji wa sheria.

Amesisitiza kuwa, mapitio hayo yanapaswa kulenga kupunguza urasimu, kurahisisha taratibu za usajili na uendeshaji wa biashara na kuvutia uwekezaji, huku yakihakikisha kuwa mifumo ya udhibiti inatekelezwa kwa ufanisi.

Amesema, mabadiliko yanayofanyika yanapaswa kuzingatia mwelekeo wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2020–2050, inayolenga kujenga uchumi shindani na jumuishi, kuongeza thamani ya bidhaa na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya taifa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa BRELA na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na utekelezaji wa majukumu ya usajili na utoaji wa leseni.

Mheshimiwa Londo ameeleza kuwa, maandalizi ya utoaji wa leseni za biashara za Daraja B kupitia mfumo wa BOS, kwa kushirikiana na TAMISEMI, ni hatua muhimu katika kuimarisha urasimishaji wa biashara nchini.

Amesema, ushirikiano huo haupaswi kuishia kwa TAMISEMI pekee, bali unapaswa kuhusisha taasisi zote zinazoweza kuchangia utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya taifa.

Mheshimiwa Londo amesema, mpango mkakati wa BRELA wa miaka mitano, kuanzia mwaka wa fedha 2026/2027 hadi 2030/2031, unapaswa kuendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa, kwa kuzingatia uboreshaji wa huduma, matumizi ya teknolojia na kuimarisha uwezo wa taasisi.

Amesisitiza kuwa, mafanikio ya mpango huo yatapimwa kwa matokeo halisi yanayoonekana kwa wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji, badala ya kuhesabu shughuli zilizotekelezwa pekee.

Aeleza umuhimu wa sekta binafsi katika uchumi

Akizungumzia mabadiliko ya mazingira ya biashara duniani, Mheshimiwa Londo amesema, nchi zinapaswa kuimarisha uwezo wa kulinda maslahi ya wananchi na kujenga mazingira yatakayowezesha biashara za ndani kukua na kushindana.

Ameeleza kuwa, uzoefu wa kimataifa unaonesha umuhimu wa Serikali kuwa na sera na mifumo inayolinda maslahi ya taifa, huku ikiendelea kuweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kufanya kazi na kuchangia maendeleo.

Vilevile, amesema Tanzania inapaswa kutumia mabadiliko ya uchumi wa dunia kama fursa ya kuimarisha uzalishaji wa ndani, kukuza viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Kwa mujibu wa Mheshimiwa Londo, BRELA ina nafasi muhimu katika kuhakikisha kuwa taratibu za usajili na uendeshaji wa biashara zinaunga mkono malengo hayo, huku zikilinda ushindani wa haki na kuhakikisha sheria zinafuatwa.

Amesisitiza kuwa, taasisi hiyo inapaswa kutumia utaalamu wake kuhakikisha kuwa mabadiliko ya sera na mifumo yanaongeza tija, yanarahisisha biashara na yanatoa mchango unaoonekana katika ukuaji wa uchumi.

Ahimiza watumishi kuzingatia mahitaji ya wananchi

Naibu Waziri Londo amewataka watumishi wa BRELA kutambua kuwa, dhamana waliyopewa ya kufanya kazi katika taasisi ya umma inaambatana na wajibu wa kuwahudumia wananchi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji.

Amesema, watumishi wanapaswa kujiona kuwa na wajibu wa kipekee wa kuwahudumia wananchi ambao hawajapata nafasi ya kuajiriwa katika Serikali, lakini wanategemea huduma za taasisi za umma katika kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

Ameonya kuwa, malalamiko ya wananchi yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito na kufanyiwa kazi, akisisitiza kuwa vikao vya watumishi havipaswi kujikita katika kujadili maslahi yao pekee bila kuangalia ubora wa huduma zinazotolewa.

Amesema, mafanikio ya taasisi yanapaswa kuonekana katika kurahisisha maisha ya wananchi, kutatua changamoto zao na kuwasaidia kutimiza malengo yao ya kiuchumi.

Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa, watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, matumizi bora ya muda, ubunifu na uwajibikaji wa pamoja.

Katika kuhimiza uwajibikaji, Mheshimiwa Londo amesisitiza umuhimu wa kila mtumishi kutekeleza sehemu yake katika kuboresha utendaji wa taasisi, akieleza kuwa mipango mizuri haina maana bila utekelezaji wenye matokeo yanayopimika.

Amesema, BRELA inapaswa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora bila kutegemea uhusiano binafsi na mtumishi fulani, ili kuimarisha uwazi, usawa na mwendelezo wa huduma hata pale watumishi wanapohama au kustaafu.

Azungumzia afya, mafao na ustawi wa watumishi

Katika kikao hicho, Mheshimiwa Londo pia amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika afya na ustawi wa watumishi, akieleza kuwa afya bora ni msingi wa kuongeza tija kazini na kuboresha utoaji wa huduma.

Amesema, magonjwa yasiyoambukiza, msongo wa mawazo na changamoto za afya ya akili ni masuala yanayohitaji kupewa kipaumbele, hasa kutokana na uhusiano wake na mtindo wa maisha, lishe na kutofanya mazoezi.

Pia, ameeleza kuwa, baadhi ya changamoto hizo zinaweza kupunguzwa kupitia elimu, maamuzi sahihi ya kiafya na kuzingatia mtindo bora wa maisha.

Amesema, Serikali hutumia rasilimali nyingi kugharamia matibabu, dawa na mafunzo ya wataalamu wa afya, hivyo kuimarisha kinga na uelewa wa afya kunaweza kusaidia kupunguza gharama hizo na kuelekeza fedha katika maeneo mengine ya maendeleo.

Mheshimiwa Londo amehimiza watumishi kutumia elimu inayotolewa kuhusu afya kama fursa ya kujenga tabia zitakazowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kuimarisha ustawi wao pamoja na familia zao.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa watumishi kupanga maisha yao ya baadaye, hususan masuala ya mafao na kustaafu, akieleza kuwa maandalizi ya maisha baada ya ajira ni muhimu kama ilivyo katika kipindi cha utumishi.

Amesema, mafunzo kuhusu mafao na wajibu wa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii, ikiwemo PSPF kama ulivyotajwa katika kikao, yanapaswa kuwasaidia watumishi kuelewa haki na wajibu wao na kupanga matumizi ya rasilimali zao kwa uangalifu.

Apongeza mpango wa kuanzisha SACCOS ya BRELA

Pia, katika kuimarisha ustawi wa watumishi, Mheshimiwa Londo ameipongeza BRELA kwa juhudi za kuanzisha Chama cha Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) akisema, hatua hiyo inaweza kusaidia kujenga utamaduni wa kuweka akiba, kuimarisha nidhamu ya matumizi na kupanua fursa za kupata huduma za kifedha.

Amesema, mipango ya kuboresha maslahi ya watumishi inapaswa kuzingatia uwezo wa kifedha wa taasisi, taratibu za utumishi wa umma na uendelevu wa shughuli za wakala.

Ameitaka menejimenti kuendelea kushughulikia hoja za watumishi kuhusu mishahara, motisha, mikopo na mazingira ya kazi kwa uwazi na kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.

Mheshimiwa Londo ameonya kuwa, matarajio na mipango isiyolingana na uwezo halisi wa kifedha yanaweza kuongeza msongo wa mawazo na kuathiri utendaji, hivyo ni muhimu kuweka malengo yanayotekelezeka na yenye kuzingatia rasilimali zilizopo.

Amesisitiza kuwa, maslahi bora kwa watumishi yanapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji, ubunifu na matokeo chanya katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aagiza maazimio ya Baraza kutekelezwa kwa wakati

Akizungumzia umuhimu wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi, Mheshimiwa Londo amesema, mafanikio ya majadiliano hayo hayapaswi kupimwa kwa idadi ya hoja zilizojadiliwa, bali kwa utekelezaji wa maazimio na matokeo yatakayopatikana katika kuboresha huduma na ustawi wa watumishi.

Naibu Waziri huyo ameitaka menejimenti kuhakikisha kuwa, kila azimio lililofikiwa linawekewa utaratibu wa utekelezaji unaobainisha hatua zinazopaswa kuchukuliwa, wahusika, muda wa kukamilisha kazi na mfumo wa kufuatilia maendeleo.

Amesema, hatua hiyo itasaidia kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha kuwa maazimio ya Baraza hayabaki katika kumbukumbu za vikao bila kuleta mabadiliko yanayotarajiwa.

Mbali na hayo, Mheshimiwa Londo ameipongeza Bodi ya Ushauri, Afisa Mtendaji Mkuu, menejimenti na watumishi wote wa BRELA kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 na kwa maandalizi ya kikao hicho.

Amewataka kuendeleza mshikamano, mawasiliano na uwajibikaji wa pamoja ili kuhakikisha kuwa taasisi inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Judith Kapinga, Mheshimiwa Londo ameahidi kuwa, wizara itaendelea kutoa ushirikiano, mwongozo na usimamizi unaohitajika ili kuiwezesha BRELA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Amesema, ushirikiano kati ya wizara na wakala huo ni muhimu katika kutatua changamoto zinazojitokeza, kuimarisha mifumo ya utoaji huduma na kuhakikisha kuwa sera na mikakati ya Serikali inatekelezwa kwa manufaa ya wananchi.

Hivyo, ametoa wito kwa wajumbe wa baraza kuhakikisha kuwa, wanarudi katika vituo vyao vya kazi wakiwa na dhamira ya kutekeleza maazimio yaliyofikiwa na kuyageuza kuwa hatua zinazoboresha utendaji wa taasisi.

Bodi ya Ushauri BRELA

Akizungumza katika kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mjumbe wa Bodi, Bw. Elias Kalist amesema kuwa, maelekezo na ushauri unaotolewa unalenga kuchochea chachu ya kuboresha utendaji kazi wa wakala huo.
"Maelekezo yanayotolewa yanalenga kutoa miongozo thabiti ya kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi wa kazi, na kuinua viwango vya utoaji huduma za wakala."

Amesema, kikao hiki cha Baraza la Wafanyakazi kimekuwa jukwaa muhimu la kutathmini utekelezaji wa majukumu ya wakala, kujadili mafanikio na changamoto, pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha ustawi wa watumishi.

Bodi hiyo imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuboresha matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za usajili na leseni nchini.

​Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo ambaye alikuwa mgeni rasmi, wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi, wawakilishi kutoka TUGHE, pamoja na viongozi na wageni waalikwa kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here