KILIMANJARO- Mkuu wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Mheshimiwa Dkt. Christopher Timbuka, amewahimiza wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.
Hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiendelea kwa vitendo mkoani Kilimanjaro.
Ameeleza kuwa, gesi ya mitungi na umeme vinapatikana katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, huku Serikali ikiwa imeweka ruzuku ili kupunguza gharama na kurahisisha upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi.
Dkt. Timbuka ameyasema hayo wakati wa zoezi la upandaji miti na utoaji wa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Soko la Sanya Juu.
Zoezi lililoandaliwa na wadau wa mazingira na nishati safi ya kupikia wa The Guardians of the Peak, kwa lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira yanayozunguka Mlima Kilimanjaro na kupunguza ukataji miti kiholela.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kupanda miti na kuitunza ili kuhakikisha uhifadhi wa mazingira unakuwa endelevu.
Kwa upande wake, Mjiolojia Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Ngereja Mgejwa amesema, elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia.
Aidha, amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Siha kuchagua na kutumia nishati safi ya kupikia inayopatikana katika maeneo yao, ikiwemo umeme, gesi na mkaa mbadala, ili kurahisisha mabadiliko ya matumizi ya nishati katika kaya zao.
Zoezi hilo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Katika kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo, wadau kutoka makundi mbalimbali walikabidhiwa mitungi ya gesi ikiwa ni motisha ya kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Tags
Dkt. Christopher Timbuka
Habari
Habari za Kilimanjaro
Mlima Kilimanjaro
Nishati Safi ya Kupikia
Uhifadhi wa Mazingira
Wilaya ya Siha





