NA DIRAMAKINI
MWENYEKITI wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Mheshimiwa Hashim Rungwe amewahimiza wakazi wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kutoa ushahidi na maoni yao mbele ya Tume ya Uchunguzi wa Kijinai kuhusu matukio ya ghasia zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Mheshimiwa Hashim Rungwe akizungumza ofisini kwake leo Oktoba 20, 2026 kuhusu umuhimu wa wananchi wa Kinondoni kujitokeza mbele ya Tume ya Jaji Lila kutoa ushahidi.Rungwe amesema, ushiriki wa wananchi katika zoezi hilo ni muhimu katika kuisaidia tume kupata taarifa sahihi kuhusu matukio yaliyotokea, huku akiwataka wazungumze kwa uhuru bila hofu wala wasiwasi.
Akizungumza leo kuhusu shughuli za tume hiyo wilayani Kinondoni, Mheshimiwa Rungwe amesema, wananchi wanaoishi katika eneo hilo wana nafasi ya kueleza kile wanachokifahamu ili kuchangia upatikanaji wa ukweli na haki.
Tume hiyo, inaendelea kuwapokea na kuwasikiliza wananchi wa Kinondoni kuanzia Oktoba 19 hadi 23, 2026 katika jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Posta jijini Dar es Salaam.
Amesisitiza kuwa, Watanzania wanapaswa kuwa na imani na tume hiyo, akieleza kuwa inajumuisha majaji na wataalamu wa sheria kutoka Tanzania na nchi nyingine, jambo alilolitaja kuwa muhimu katika kuimarisha uchunguzi.
“Ninawahimiza wananchi wa Kinondoni kujitokeza na kutoa maoni yao kuhusu yote yaliyotokea katika kipindi hicho. Mnapaswa kuwa huru kueleza ukweli bila wasiwasi, kwa sababu kwa kufanya hivyo mtakuwa mmeisaidia nchi kupata taarifa muhimu,” amesema Mheshimiwa Rungwe.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa hiyo kushiriki katika mchakato wa uchunguzi, akieleza matumaini yake kuwa tume itawasilisha ripoti inayozingatia haki na ukweli.
Tume hiyo iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande iliyowasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026. Inaongozwa na Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mheshimiwa Shabani Ally Lila.
Wajumbe wengine ni Naibu Jaji Mkuu wa Namibia, Mheshimiwa Petrus Tileinge Damaseb; Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Uganda, Cheborion Barishaki; pamoja na majaji wastaafu Watanzania Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Tume hiyo ina jukumu la kuchunguza matukio ya ghasia zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa lengo la kubaini ukweli kuhusu matukio hayo na kuwasilisha matokeo ya uchunguzi wake.
Tags
BoT
CHAUMMA
Habari
Habari za Siasa Tanzania
Hashim Rungwe
Tume ya Jaji Lila
Vurugu za Uchaguzi 2025
Wilaya ya Kinondoni