NA DIRAMAKINI
MBUNGE wa Jimbo la Kinondoni jijini Dar Es Salaam, Mheshimiwa Abbas Tarimba amewahimiza wakazi wa wilaya hiyo kujitokeza kutoa ushahidi na taarifa wanazozifahamu kwa Tume ya Uchunguzi wa Kijinai kuhusu matukio ya ghasia zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Mheshimiwa Abbas Tarimba akizungumza leo kuhusu Tume ya Jaji Lila.
Mheshimiwa Tarimba ametoa wito huo leo, wakati tume hiyo ikiendelea kupokea ushahidi kutoka kwa wananchi wa Kinondoni kwa muda wa wiki moja katika ofisi zilizopo kwenye jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) eneo la Posta jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa zoezi hilo, Mbunge huyo amesema, ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kusaidia uchunguzi kubaini mazingira yaliyozunguka matukio ya Oktoba 29, 2025, ambayo kwa mujibu wake, yalisababisha vifo, upotevu wa mali na baadhi ya watu kutoweka.
Amesema, matukio hayo yaliibua hali ya hofu na taharuki miongoni mwa wakazi, hivyo amewataka wenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi kuziwasilisha kwa tume ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi.
“Nawaomba wananchi wenzangu wa Kinondoni, ikiwa una taarifa yoyote inayoweza kusaidia tume kubaini waliohusika kupanga, kutekeleza au kufadhili matukio hayo, jitokeze kutoa ushahidi wako. Tufanye hivyo kwa lengo la kuisaidia nchi yetu kupata ukweli na kuimarisha amani na utulivu,” amesema Tarimba.
Ameongeza kuwa, ushirikiano wa wananchi unaweza kusaidia tume kupata maelezo muhimu kuhusu matukio hayo, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa zinazotegemea kile walichokiona, kukisikia au kukifahamu.
Tume hiyo iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande, iliyowasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026. Inaongozwa na Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Shabani Ally Lila.
Wajumbe wengine ni Naibu Jaji Mkuu wa Namibia, Petrus Tileinge Damaseb; Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Uganda, Cheborion Barishaki; pamoja na majaji wastaafu wa Tanzania Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Tume hiyo ina jukumu la kuchunguza ghasia zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili kubaini ukweli kuhusu matukio hayo na kuwasilisha matokeo ya uchunguzi.
Kabla ya kuanza kupokea ushahidi kutoka kwa wakazi wa Kinondoni, tume ilikuwa imesikiliza wananchi wa wilaya za Ilala, Kigamboni, Temeke na Ubungo. Wananchi wa maeneo hayo wanaendelea kuwa na fursa ya kuwasilisha taarifa wanazozifahamu ana kwa ana au kupitia simu au barua pepe.
Tags
Abbas Tarimba
BoT
Habari
Habari za Siasa Dar es Salaam
Jimbo la Kinondoni
Tume ya Jaji Lila
Vurugu za Uchaguzi 2025
