NA GODFREY NNKO
WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) umewataka wafanyabiashara kutumia vipimo sahihi na vilivyohakikiwa kisheria ili kuhakikisha wanunuzi wanapata kiasi halisi cha bidhaa wanazolipia, huku ukisisitiza kuimarisha ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya biashara nchini.
Elimu ya vipimo kwa wananchi imeendelea kuwa kipaumbele kikubwa cha Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA).Wito huo umetolewa na Meneja wa Sehemu ya Ukaguzi na Ufuatiliaji wa WMA, Bw. Jadi Athumani leo Oktoba 20, 2026 katika mahojiano maalumu kupitia kipindi cha Baragumu kinachorushwa na Channel Ten jijini Dodoma, alipokuwa akieleza umuhimu wa vipimo sahihi katika kukuza biashara na kuchochea maendeleo endelevu.
Bw. Athumani amesema, vipimo vya uhakika ni vile vinavyohakikisha kiasi kinachotolewa kinaendana na thamani inayotakiwa, hivyo ni wajibu wa wafanyabiashara kuhakikisha wanatumia vifaa vinavyokidhi matakwa ya sheria.
Amesema, changamoto ya vipimo visivyo sahihi inaweza kujitokeza hata kwa wafanyabiashara wadogo wanaouza bidhaa kwa kutumia visado, hali inayoweza kusababisha mnunuzi kukosa kiwango kinacholingana na fedha alizolipa.
Meneja huyo ametoa mfano wa wauzaji wa nyanya, vitunguu na bidhaa nyingine wanaopanga bidhaa zao kando ya barabara, akisema ni muhimu kuhakikisha visado vinavyotumika vinatoa kiasi kinachokidhi thamani iliyokusudiwa badala ya kutegemea makadirio ya macho.
Aamesisitiza kuwa, wafanyabiashara wanapaswa kutumia vipimo vinavyoweza kuhakikiwa ili kulinda maslahi yao na ya wateja, pamoja na kujenga imani katika shughuli za kibiashara.
WMA yahakiki bidhaa zilizofungashwa
Akizungumzia malalamiko ya wateja kuhusu bidhaa zinazouzwa zikiwa zimefungashwa, ikiwemo unga, Bw. Athumani amesema, WMA ina jukumu la kukagua bidhaa hizo ili kuhakikisha kiasi kilichoandikwa kwenye vifungashio kinaendana na kilichomo ndani.
Ameeleza kuwa, ukaguzi huo hufanyika katika maeneo rasmi ya uzalishaji na ufungashaji wa bidhaa, kupitia ofisi za WMA zilizopo katika mikoa mbalimbali nchini.
Pia, ukaguzi huo ni sehemu ya shughuli za kawaida za wakala, huku ukaguzi wa kushtukiza ukifanyika mara kwa mara ili kubaini kama bidhaa zilizokaguliwa zinaendelea kukidhi viwango vinavyotakiwa.
Aidha, amesema mizani inayotumiwa na wafanyabiashara wa rejareja hukaguliwa ili kuthibitisha usahihi wake kabla ya kutumika kuwahudumia wateja.
Amebainisha kuwa, mizani hiyo hukaguliwa kwa mujibu wa ratiba za ukaguzi zinazotekelezwa katika mikoa mbalimbali, na inapothibitishwa kuwa inakidhi matakwa ya kisheria huwekewa alama au stika ya uhakiki.
Bw. Athumani amewataka walaji kuangalia alama hiyo wanapotumia mizani katika maeneo ya biashara na kutoa taarifa kwa ofisi za WMA zilizo karibu nao wanapobaini vifaa visivyo na alama ya uhakiki.
Vituo vya mafuta kukaguliwa kwa ratiba na kushtukiza
Kuhusu malalamiko ya baadhi ya watumiaji wa magari wanaodai kupata tofauti ya matumizi ya mafuta wanaponunua katika vituo mbalimbali, Bw. Athumani amesema, pampu za mafuta pia hukaguliwa ili kuhakikisha zinatoa kiasi kinacholingana na malipo ya mteja.
Amesema, ukaguzi wa vituo vya mafuta hufanyika kwa ratiba maalumu, huku wamiliki wakipewa taarifa kabla ya ukaguzi wa kawaida wa mwaka.
Hata hivyo, amefafanua kuwa, WMA hufanya pia ukaguzi wa kushtukiza ili kujiridhisha kuwa pampu zote zinaendelea kufanya kazi kwa usahihi na kutoa kiwango kinachostahili.
Ameongeza kuwa, malalamiko yanapopokelewa kutoka kwa wananchi, wakala huchukua hatua za kufuatilia taarifa hizo na kufanya ukaguzi pale inapohitajika.
Bw. Athumani amesema, pampu zinazohakikiwa huwekewa stika inayoonesha mwezi na mwaka wa ukaguzi, ikiwa ni njia ya kumwezesha mtumiaji kutambua kuwa kifaa husika kimepitia utaratibu wa uhakiki.
Amewataka wananchi wanaohisi wamepatiwa mafuta pungufu kuwasiliana na ofisi ya WMA katika maeneo yao ili wataalamu wafike na kuchunguza malalamiko hayo.
Hata hivyo, amewakumbusha watumiaji wa magari kuwa tofauti katika usomaji wa geji za mafuta inaweza pia kusababishwa na hitilafu za mifumo ya magari, hivyo ni muhimu kujiridhisha kuhusu hali ya kifaa hicho kabla ya kuhitimisha kuwa kituo cha mafuta kimetoa kiwango pungufu.
WMA yaimarisha udhibiti wa rumbesa
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa kudhibiti matumizi ya rumbesa katika biashara ya mazao, Bw. Athumani amesema wakala umeweka vituo vya huduma katika maeneo muhimu yanayohusika na malalamiko kuhusu vipimo vya mazao.
Pia, amesema wakaguzi wamekuwa wakihudumu katika vituo hivyo asubuhi, mchana na jioni ili kuhakikisha mazao yanayopimwa na kuuzwa yanazingatia matakwa ya sheria.
Amefafanua kuwa, rumbesa haiwezi kutambuliwa kwa kutegemea mwonekano wa nje pekee, bali kwa kuzingatia kiasi kinachozidi kiwango kinachoruhusiwa kwa mujibu wa utaratibu wa vipimo.
Meneja huyo amesema, baadhi ya watu wamekuwa wakihusisha rumbesa na kishungi kinachoonekana juu ya gunia la mazao, lakini mwonekano huo pekee hautoshi kuthibitisha kuwa kuna ukiukwaji wa vipimo.
Kwa mantiki hiyo, amesisitiza umuhimu wa kutumia vipimo sahihi ili kubaini kiasi halisi cha mazao na kuepusha mazingira yanayoweza kumwathiri mkulima au mnunuzi.
Bw. Athumani amewahimiza wakulima kupima mazao yao wanapoyatoa shambani ili kufahamu kiasi halisi wanachozalisha na kuhakikisha wanapouza wanapata malipo yanayolingana na bidhaa wanazowasilisha sokoni.
Amesema, uelewa kuhusu vipimo sahihi ni muhimu kwa pande zote mbili za biashara, kwa kuwa kutokufahamu kiasi halisi kunaweza kusababisha mkulima kudhulumiwa au mnunuzi kupata bidhaa pungufu.
WMA yafuatilia malalamiko ya mitungi ya gesi
Katika hatua nyingine, Bw. Athumani amesema, WMA imekuwa ikifuatilia malalamiko ya wananchi kuhusu mitungi ya gesi inayodaiwa kuisha haraka baada ya kununuliwa.
Amesema, baada ya malalamiko kusambaa kupitia mitandao ya kijamii, wakala uliwaelekeza mameneja wa mikoa kufanya ukaguzi ili kubaini kama madai hayo yana msingi.
Mbali na hayo amesema, ukaguzi uliofanyika ulibaini kuwa, baadhi ya malalamiko yalikuwa ya msingi, huku mengine yakiwa hayajathibitishwa kuwa na changamoto ya vipimo.
Amesema, hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutambua kiasi cha bidhaa wanazonunua na hatua za kuchukua wanapohisi kuwa wamepata kiwango kisicholingana na malipo yao.
Bw. Athumani amesisitiza kuwa, mitungi ya gesi ni bidhaa inayopaswa kuzingatia vipimo vinavyotakiwa, hivyo watumiaji wanapaswa kuwa na uelewa wa haki zao na kutoa taarifa wanapobaini viashiria vya ukiukwaji.
Ameongeza kuwa, WMA itaendelea kutekeleza majukumu yake ya ukaguzi, ufuatiliaji na utoaji wa elimu kwa umma ili kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara vinakuwa sahihi na vinazingatia sheria kote nchini.Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) ni taasisi ya Serikali ambayo ipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo ilianzishwa rasmi Mei 20, 2002 ikiwa na jukumu kuu la kuwalinda walaji kupitia matumizi sahihi ya vipimo.
Tags
Habari
Habari za Biashara Tanzania
Jadi Athumani
Udhibiti wa Rumbesa
Uhakiki wa Vipimo
Ulinzi wa Walaji
Vituo vya Mafuta
Wakala wa Vipimo Tanzania WMA
