DODOMA- Mgeni rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari amesisitiza umuhimu wa kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili kulinda maisha na mali za wananchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao hicho Oktoba 19, 2026 kwenye Ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.
Jaji Mshibe ameyasema hayo Oktoba 19, 2026 wakati akifungua kikao cha wadau kutoka sekta mbalimbali kilichofanyika katika ukumbi wa PSSSF, Dodoma kwa ajili ya kujadili athari na ushauri kwa kila sekta. Hii ni moja ya hatua za maandalizi ya kutoa Utabiri wa Mvua za Msimu Novemba, 2026 hadi Aprili 2027.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari akifungua kikao cha wadau kutoka sekta mbalimbali nchini.Akizungumzia hatua za kukabiliana na maafa amesisitiza kuwa, uokozi wenye tija ni ule unaofanyika kabla athari hazijatokea, hapo unakuwa umeiokoa jamii, na mwisho alitoa wito kwa wadau kutumia tahadhari za hali ya hewa kupanga hatua za kinga na kujiandaa mapema, badala ya kusubiri maafa yatokee.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia Nchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a amesisitiza, umuhimu kwa wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia utabiri na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa.
"Kama tulivyoeleza katika utabiri tulioutoa tarehe 18 Agosti 2026, tunatarajia unyeshaji wa mvua kuendelea kuimarika zaidi kuelekea mwishoni mwa mwezi huu na hususani mwezi Novemba."
Kikao hicho kilibeba kaulimbiu: “Kupunguza Pengo la Uelewa wa Tahadhari za Hali ya Hewa kwa Pamoja,” kikilenga kuimarisha uelewa na ushirikiano wa wadau katika matumizi na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa.
Utabiri wa Mvua za Msimu wa Novemba 2026 hadi Aprili 2027 unatarajiwa kutolewa rasmi Oktoba 23, 2026 ukitanguliwa na warsha za wahariri na waandishi wa habari.
Tags
Dkt. Ladislaus Chang'a
Habari
Habari za Mazingira Tanzania
Jaji Mshibe Ali Bakari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Mvua za Msimu 2026
Utabiri wa Hali ya Hewa


