WMA yafafanua jinsi Vipimo Sahihi vinavyolinda walaji na kusaidia TRA kukusanya mapato

NA GODFREY NNKO

WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) umefafanua kuwa, jukumu lake kuu ni kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii vinakuwa sahihi na vinatoa matokeo yanayoaminika, hatua inayolenga kulinda haki za walaji, wafanyabiashara na Serikali.
Meneja wa Sehemu ya Ukaguzi na Ufuatiliaji wa WMA, Bw. Jadi Athumani.

Wakala huo pia, unahusika na uhakiki wa vipimo vya ujazo na mtiririko wa vimiminika ikiwemo mafuta yanayoingizwa nchini, pamoja na ukaguzi wa magari yanayosafirisha mchanga na vifaa vingine vya ujenzi ili kubaini kiasi halisi cha mizigo inayobebwa.

Meneja wa Sehemu ya Ukaguzi na Ufuatiliaji wa WMA, Bw. Jadi Athumani ameyasema hayo leo Oktoba 20, 2026 jijini Dodoma, wakati wa mahojiano maalumu katika kipindi cha Baragumu kinachorushwa na Channel Ten, alipokuwa akielezea umuhimu wa vipimo vya uhakika katika kuchochea maendeleo endelevu.

Amesema, kuna dhana inayoweza kuwepo miongoni mwa wananchi kwamba WMA inasimamia moja kwa moja shughuli za biashara, wakati jukumu lake la msingi ni kuhakiki na kukagua vipimo vinavyotumika katika shughuli hizo ili kuhakikisha vinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Pia, amefafanua kuwa, kila kipimo kinachotumika kumhudumia mlaji kinapaswa kutoa matokeo sahihi ili mnunuzi apate bidhaa kulingana na kiasi alicholipia.

Kwa mfano, amesema mtu anaponunua mchele kwa kipimo cha kilo moja, ni wajibu wa WMA kuhakikisha mizani inayotumika inatoa uzito sahihi.

Halikadhalika, katika ununuzi wa mafuta ya petroli au dizeli, pampu za mafuta zinapaswa kuonesha kiasi halisi kinachotolewa kwa mteja.

Amesisitiza kuwa, uhakiki huo ni muhimu katika kuimarisha imani ya wananchi katika shughuli za kibiashara na kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya vipimo visivyo sahihi.

Uhakiki wa ujazo na mtiririko

Akizungumzia vipimo vya ujazo na mtiririko, Bw. Athumani amesema, WMA hufanya uhakiki ili kubaini kiasi halisi cha vitu vinavyopimwa au kupitishwa katika mifumo maalumu, kutegemea aina ya kipimo kinachohusika.

Ameeleza kuwa, kipimo cha ujazo hutumika kubaini kiasi halisi cha kitu kilichomo ndani ya chombo, tenki au gari maalumu la kubebea mizigo.

Kwa upande mwingine, kipimo cha mtiririko hutumika kubaini kiasi cha kimiminika kinachopita katika mfumo fulani ndani ya kipindi maalumu.

Bw. Athumani amesema, WMA hukagua magari yanayosafirisha mchanga, kokoto na vifaa vingine vya ujenzi ili kubaini ujazo wake halisi.

Hatua hiyo, amesema husaidia kujua kiasi cha vifaa vinavyosafirishwa na hivyo kuongeza uwazi katika shughuli za usafirishaji na biashara ya vifaa hivyo.

Amesema, ukaguzi huo unahitaji vipimo sahihi vya magari husika ili kubaini uwezo wake wa kubeba mzigo na kiasi halisi cha mchanga au kokoto kilichomo.
Meneja huyo amesema, WMA ina kituo cha kuhakiki magari ya kusafirishia mafuta kilichopo Misugusugu mkoani Pwani, ambako uhakiki hufanyika ili kubaini ujazo wa mafuta yanayobebwa katika magari hayo.

Amefafanua kuwa, uhakiki huo ni muhimu katika kuhakikisha kiasi cha mafuta kinachopokelewa na kusafirishwa kinaweza kubainishwa kwa usahihi, jambo linalosaidia kuongeza uwazi katika mnyororo wa usambazaji wa bidhaa hiyo.

Vipimo sahihi vyasaidia ukusanyaji wa mapato

Bw. Athumani amesema, jukumu la WMA katika kuhakiki mtiririko wa mafuta yanayoingia nchini lina mchango muhimu katika kuwezesha mamlaka husika kupata takwimu sahihi za kiasi cha mafuta kinachoingizwa nchini.

Amesema, taarifa hizo zinaweza kutumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kutekeleza majukumu yake ya kikodi kwa kuzingatia kiasi halisi cha mafuta kilichoingizwa nchini.

Vilevile ameeleza kuwa, vipimo sahihi katika hatua za upokeaji na usambazaji wa mafuta vinasaidia kupunguza uwezekano wa tofauti za takwimu, kuimarisha uwazi na kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa kuzingatia taarifa zinazotegemewa.

Akifafanua zaidi kuhusu maana ya mtiririko amesema, ni kipimo kinachohusisha kiasi cha kimiminika kinachopita katika mfumo fulani kama vile mafuta au maji.

Meneja huyo amesema, uhakiki wake ni muhimu katika kubaini kiasi kinachopita katika mifumo ya kupokea, kusafirisha au kusambaza vimiminika hivyo.

Kwa upande wa ujazo amesema, dhana hiyo inalenga kubaini kiasi halisi cha kitu kilichomo ndani ya chombo au sehemu inayopimwa.

Amesisitiza kuwa, usahihi wa vipimo katika sekta mbalimbali ni sehemu muhimu ya kulinda maslahi ya wananchi na kuwezesha shughuli za kiuchumi kutekelezwa kwa uwazi, uwajibikaji na ufanisi.

Meneja huyo amesisitiza kuwa, WMA inalenga kuhakikisha vipimo vinavyotumika nchini vinaaminika na vinakidhi mahitaji ya matumizi yaliyokusudiwa, hatua inayochangia kulinda walaji na kuimarisha mifumo ya biashara na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Wakala wa Vipimo ni taasisi ya Serikali ambayo ipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo ilianzishwa rasmi Mei 20, 2002 ikiwa na jukumu kuu la kuwalinda walaji kupitia matumizi sahihi ya vipimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here