DODOMA- Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma leo Oktoba 20, 2026 imeshinda kesi ya uhujumu uchumi iliyomhusu Thabiti Yusufu Ngulungu, aliyekuwa Afisa Hesabu Msaidizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba na ambaye kwa sasa ni Afisa Hesabu Msaidizi katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kondoa.
Mahakama imemhukumu mshtakiwa kulipa faini ya shilingi 50,000 na kurejesha fedha za fidia kiasi cha shilingi 3,600,200 kwa ajili ya wahanga walioathirika.
Ni baada ya Mahakama ya Wilaya ya Chemba kumtia hatiani kwa kosa la wizi wa fedha za mauzo ya viwanja kiasi cha shilingi 3,600,200.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa, kati ya Januari 8 na Desemba 30, 2020, mshtakiwa alipokea fedha za mauzo ya viwanja kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mombose, John Wenga, lakini aliwasilisha kwa Mtunza Fedha wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, fedha pungufu ya kiasi kilichopaswa kuwasilishwa.
Kitendo hicho kilikuwa kinyume na masharti ya kifungu cha 50(5) cha Randama ya Fedha za Serikali za Mitaa ya mwaka 2009.
Kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi Na. 19251/2026, Jamhuri dhidi ya Thabiti Yusufu Ngulungu, ilisikilizwa na Mheshimiwa Andrew Hayuma, Hakimu Mkazi Mfawidhi, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Mawakili wa Serikali Dickson Misanjo na Happiness Mfungo kutoka TAKUKURU Mkoa wa Dodoma.
Katika uamuzi wake wa leo Oktoba 20, 2026, mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kwa kosa moja la wizi uliofanywa na mtumishi wa umma, kinyume na vifungu vya 258(1) na 270 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Toleo la mwaka 2023.
Mahakama imemhukumu mshtakiwa kulipa faini ya shilingi 50,000 na kurejesha fedha za fidia kiasi cha shilingi 3,600,200 kwa ajili ya wahanga walioathirika.
Mshtakiwa ametekeleza hukumu hiyo kwa kulipa faini na kurejesha fedha zote za fidia zilizoamriwa na mahakama.
Tags
Habari
Habari za Mahakama Dodoma
Halmashauri ya Chemba
Kesi ya Wizi Chemba
TAKUKURU Dodoma
Thabiti Yusufu Ngulungu
Uhujumu Uchumi
