Tume ya Jaji Lila yafika Temeke, yawaita wananchi kutoa ushahidi Chuo cha DUCE

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Tume ya Rais ya Kuchunguza Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria katika Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mheshimiwa Shaban Ally Lila,l amewataka wananchi wa Wilaya ya Temeke kujitokeza na kutoa taarifa na ushahidi kuhusu matukio ya ghasia na ukiukwaji wa sheria yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi huo.
Jaji Lila amesema, tume hiyo kwa sasa inaendelea na kazi zake katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, ambapo shughuli za ukusanyaji wa taarifa na ushahidi zinafanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), kilichopo Chang’ombe.

Akizungumza leo, Jaji Lila amesema, Tume tayari imekamilisha shughuli zake katika wilaya za Kigamboni na Ilala na sasa imeelekeza shughuli zake katika Wilaya ya Temeke kwa ajili ya kukusanya taarifa zitakazosaidia kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa hadidu za rejea.

“Tunawakaribisha wananchi wote wenye taarifa zozote zinazoweza kuisaidia Tume katika kutekeleza majukumu yake kama ilivyobainishwa kwenye hadidu za rejea,” amesema Jaji Lila.

Amesema, Tume pia inawakaribisha wananchi waliopata madhara kutokana na matukio ya ghasia na vurugu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi huo, ili kutoa ushahidi kuhusu matukio waliyoyaona, kuyafahamu au kuyapitia.

Kwa mujibu wa Jaji Lila, Tume inalenga pia kupata taarifa zitakazosaidia kubaini watu waliohusika katika kupanga, kuratibu, kufadhili na kutekeleza matukio hayo ya vurugu.

Aidha, amewahakikishia wananchi wanaojitokeza kutoa ushahidi kuwa usalama wao na usiri wa taarifa watakazozitoa utalindwa.

“Kwa wale wote watakaojitokeza, tunawahakikishia kwamba taarifa zao zitatumiwa na Tume kwa usiri mkubwa,” amesema.

Amesema, wananchi ambao hawawezi kufika moja kwa moja katika eneo la Tume wanaweza kuwasilisha taarifa zao kupitia namba ya simu 0733 730 544 au barua pepe barua@tumeuchunguzi.go.tz.

Jaji Lila amewahimiza wananchi wa Temeke kutumia fursa hiyo kutoa taarifa walizonazo ili kuisaidia Tume katika kutekeleza jukumu ililopewa la kuchunguza matukio ya ghasia na ukiukwaji wa sheria yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here