NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa, kushindwa kurejesha mikopo midogo inayotolewa kupitia mitandao ya simu za mkononi kama Songesha kunaweza kuathiri sifa ya mkopaji na kupunguza uwezekano wa kupata mikopo mikubwa katika taasisi za fedha.
Pia, imebainisha kuwa, ukosefu wa dhamana ya kutosha na historia isiyoridhisha ya urejeshaji wa mikopo ni miongoni mwa changamoto zinazowakwamisha wajasiriamali na wafanyabiashara kupata mikopo kutoka katika benki na taasisi za fedha nchini.
Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Fedha BoT, Bi. Gloria Chellunga ameyasema hayo Novemba 5, 2026 wakati akiwasilisha mada kuhusu jinsi Mfumo wa Dhamana ya Mikopo unavyofanya kazi na wigo wake wa kisheria, katika semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema, Serikali imeanzisha mifuko miwili ya dhamana ya mikopo inayosimamiwa na BoT kwa lengo la kuwasaidia wajasiriamali wenye miradi yenye tija ambao wanakosa mikopo kutokana na upungufu wa dhamana.
Bi. Chellunga amesema mifuko hiyo ni Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Mauzo ya Nje (Export Credit Guarantee Scheme - ECGS), ulioanzishwa Julai 2002, na Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (Small and Medium Enterprises Credit Guarantee Scheme - SMECGS), ulioanzishwa Septemba 2005.
Amesema, lengo la mifuko hiyo ni kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara wenye miradi inayokidhi vigezo vya ukopeshaji kupata mikopo kupitia dhamana ya Benki Kuu pale wanapokuwa na upungufu wa mali zinazohitajika kuwekwa rehani.
Pia, amefafanua kuwa dhamana ya mkopo ni mali au kitu chenye thamani kinachowekwa na mkopaji ili kuhakikisha kuwa mkopo aliouchukua unarejeshwa.
"Endapo mkopaji atashindwa kutimiza wajibu huo, taasisi ya fedha inaweza kuchukua hatua za kisheria za kuuza mali iliyowekwa dhamana ili kurejesha fedha ilizokopesha."
Amesema, utaratibu huo ni muhimu kwa sababu benki hukopesha fedha zinazotokana na amana za wateja, hivyo zina wajibu wa kuhakikisha usalama wa fedha hizo na uwezo wa wakopaji kurejesha mikopo.
Hata hivyo, amesema baadhi ya wajasiriamali wamekuwa wakishindwa kukidhi masharti ya dhamana licha ya kuwa na miradi yenye uwezo wa kujiendesha na kuleta faida, jambo lililosababisha Serikali kuanzisha mifuko hiyo ili kuziba pengo lililopo.
Dhamana inayotolewa na Serikali
Akielezea utaratibu wa dhamana chini ya mfuko wa ECGS, Bi. Chellunga amesema, Benki Kuu inaweza kudhamini hadi asilimia 75 ya mkopo unaolipwa ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja, huku mikopo inayolipwa kwa zaidi ya mwaka mmoja ikiweza kupata dhamana ya hadi asilimia 50 ya thamani ya mkopo.
Amesema, dhamana hiyo haimaanishi kuwa Benki Kuu inatoa fedha za mkopo moja kwa moja kwa mjasiriamali, bali inahakikisha taasisi ya fedha inayokopesha inalindwa kwa sehemu ya kiasi cha fedha inachokopesha endapo mkopaji atashindwa kurejesha.
Kwa upande wa SMECGS amesema, mkopo unaoweza kupata dhamana kupitia mfuko huo ni kuanzia Shilingi milioni 50 hadi Shilingi bilioni moja, huku muda wa marejesho ukiwa hadi miaka mitano kwa mikopo inayotolewa na benki za biashara na hadi miaka saba kwa mikopo inayotolewa na benki za maendeleo.
Mchambuzi huyo ameeleza kuwa, mfuko huo unadhamini asilimia 50 ya mkopo mkuu pekee, bila kujumuisha riba na gharama nyingine zinazotozwa na taasisi ya fedha.
Masharti ya kunufaika na mifuko hiyo
Bi. Chellunga amesema, ili mjasiriamali anufaike na mifuko hiyo, ni lazima awe Mtanzania, huku kampuni inayotafuta dhamana ikitakiwa kuwa na umiliki wa Watanzania wa angalau asilimia 50 ya hisa zake.
Amesema, mradi unaoombewa mkopo unapaswa kuwa na tija kiuchumi, kuongeza ajira na kipato, pamoja na kuchochea uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma.
Vilevile, amefafanua kuwa chini ya mfuko wa ECGS, dhamana inalenga zaidi miradi inayozalisha bidhaa kwa ajili ya kuuzwa katika masoko ya nje ya nchi ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
Aidha, miradi inayozalisha bidhaa ndani ya nchi ambazo awali zilikuwa zikiagizwa kutoka nje inaweza kunufaika kwa kuwa uzalishaji huo unapunguza utegemezi wa bidhaa za kutoka nje na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.
Amesisitiza kuwa, mradi unaoombewa dhamana lazima uwe na usimamizi wenye utaalamu na uzoefu katika shughuli husika ili kuongeza uwezekano wa kufanikiwa na kurejesha mkopo.
Hata hivyo, amebainisha kuwa si kila mjasiriamali anayehitaji mkopo anaweza kuwasilisha ombi la dhamana moja kwa moja Benki Kuu. Kwanza, taasisi ya fedha inapaswa kufanya tathmini na kujiridhisha kuwa mradi unakidhi vigezo vya kukopesheka, lakini mwombaji ana upungufu wa dhamana.
Amesema, Serikali inaingilia kati katika mazingira hayo pekee, na si pale ambapo benki imekataa kutoa mkopo kutokana na sababu nyingine za kibiashara au kutokidhi masharti ya ukopeshaji.
Historia ya mikopo ina umuhimu
Akizungumzia umuhimu wa taarifa za wakopaji, Bi. Chellunga amesema, benki na taasisi za fedha hutumia taarifa zinazohifadhiwa na taasisi za kumbukumbu za wakopaji (Credit Reference Bureau) kutathmini historia na nidhamu ya kifedha ya mtu anayeomba mkopo.
Amesema, taarifa hizo huonesha mwenendo wa mkopaji katika kurejesha mikopo aliyowahi kuchukua kutoka benki, taasisi za fedha na hata kampuni za huduma za kifedha zinazotumia mitandao ya simu za mkononi.
Bi. Chellunga ametoa mfano wa mtu anayekopa kiasi kidogo cha fedha kupitia huduma kama Songesha na kushindwa kurejesha kwa wakati, akieleza kuwa taarifa hiyo inaweza kuathiri tathmini ya uwezo na uaminifu wake katika kukopa.
Amesema, taasisi za fedha hazitazami tu kiasi cha fedha ambacho mtu ameshindwa kurejesha, bali pia hutathmini mwenendo wake wa kifedha ikiwemo utayari na uwezo wa kutimiza wajibu wa marejesho.
Bi. Chellunga amesisitiza kuwa, historia mbaya ya mikopo inaweza kuwa kikwazo kwa mjasiriamali kupata dhamana kupitia mifuko hiyo, hata kama ana mradi mzuri na mali alizonazo hazitoshelezi dhamana inayohitajika.
Utaratibu wa kuomba dhamana
Akifafanua hatua za kupata dhamana, Bi. Chellunga amesema, mjasiriamali anapaswa kuanza kwa kuwasilisha maombi ya mkopo katika benki au taasisi ya fedha yenye leseni na inayosimamiwa na Benki Kuu kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
Amesema, mwombaji anatakiwa kuwasilisha nyaraka zote zinazohitajika na taasisi husika, zikiwemo taarifa za mradi na vielelezo vingine vinavyothibitisha uwezo wa biashara kujiendesha na kurejesha mkopo.
Baada ya kupokea maombi, benki hufanya tathmini ya mradi, uwezo wa mwombaji kurejesha fedha na historia yake ya mikopo kabla ya kuamua kama anastahili kukopeshwa.
Endapo benki itaridhika kuwa mradi unakidhi masharti ya ukopeshaji, lakini mwombaji ana upungufu wa dhamana, taasisi hiyo ndiyo inayowasilisha maombi ya dhamana Benki Kuu kwa niaba ya mteja.
Amesema, utaratibu huo unaweka wazi kuwa dhamana ya Serikali kupitia mifuko hiyo si mbadala wa masharti ya kawaida ya mikopo, bali ni nyenzo ya kusaidia wajasiriamali wanaokidhi vigezo vya ukopeshaji lakini wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na dhamana ya kutosha.
Bi. Chellunga amewahimiza wafanyabiashara na wajasiriamali kuzingatia nidhamu ya fedha, kurejesha mikopo kwa wakati na kuhakikisha wanakuwa na taarifa nzuri za mikopo ili kuongeza nafasi ya kupata mitaji kupitia benki na taasisi za fedha nchini.


