BoT: Kutupa Noti chini na kuzikanyaga kwenye sherehe kunaharibu fedha, kuisababishia Serikali hasara

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya noti na sarafu za fedha za Tanzania, ikieleza kuwa, vitendo vya kuzitupa chini, kuzikanyaga na kuziharibu katika shughuli za kijamii na burudani vinasababisha hasara kubwa kwa taifa.
Wito huo umetolewa na Meneja Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano ya Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Noves Moses leo Novemba 6, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari za uchumi na masoko ya fedha yaliyoandaliwa na benki hiyo.

Bi. Moses amesema, kumekuwa na ongezeko la tabia zisizofaa za matumizi ya fedha, hususan katika sherehe na shughuli mbalimbali za kijamii, ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakitupa noti chini, kuzikanyaga na kuzitumia kwa namna inayozifanya kuharibika ndani ya muda mfupi.

Amesema, hali hiyo inaleta gharama kwa Benki Kuu, ambayo inawajibika kusimamia mchakato mzima wa upatikanaji wa fedha, kuanzia kubaini mahitaji ya noti na sarafu, kuziagiza, kuzisambaza hadi kuziondoa katika mzunguko wa matumizi zinapokuwa zimeharibika.

Bi. Moses ameeleza kuwa, baadhi ya noti mpya zinazotupwa chini wakati wa sherehe na shughuli za burudani huishia kuchakaa na kushindwa kutumika katika mashine za kuhesabia fedha, hivyo kulazimika kuondolewa katika mzunguko na kubadilishwa, jambo linalosababisha hasara isiyokuwa ya lazima.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Bi. Moses amesema, Benki Kuu imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo wasanii, waandaaji wa shughuli za kijamii na wasimamizi wa sherehe ili kuhamasisha matumizi yanayozingatia thamani na heshima ya fedha.

Amesema, benki hiyo imekuwa ikiwasiliana pia na watangazaji wa shughuli mbalimbali (MCs), ambao wana nafasi ya kuwafikia watu wengi na kuhamasisha utunzaji wa fedha wakati wa sherehe na burudani.

Ameongeza kuwa, wananchi wanaotaka kuchangia au kuonesha furaha kwa kutumia fedha katika shughuli mbalimbali wanapaswa kuweka noti hizo kwenye vikapu, vyombo maalumu au sehemu zilizotengwa badala ya kuzitupa sakafuni na kuzifanya zikanyagwe.

Bi. Moses amesema, Benki Kuu imejikita zaidi katika kutoa elimu kwa umma kuliko kuanza na hatua za adhabu, kwa kuwa inaamini bado kuna haja ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha na madhara ya kuziharibu.

Amesema, elimu hiyo hutolewa kupitia maonesho mbalimbali, masoko na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu, hususan sehemu ambazo matumizi ya fedha taslimu ni makubwa.

Katika hatua nyingine, amewahimiza wananchi kutumia zaidi mifumo ya malipo ya kielektroniki badala ya kutegemea fedha taslimu pekee, akieleza kuwa teknolojia ya malipo imeendelea kurahisisha shughuli mbalimbali za kifedha.

Meneja huyo ametaja baadhi ya njia hizo kuwa ni malipo kwa kutumia kadi, kuchanganua misimbo ya malipo (QR codes) na teknolojia ya kugusa kadi au kifaa cha malipo (contactless payments) ambazo zinaweza kupunguza matumizi ya noti katika miamala ya kila siku.

Hata hivyo, amesema wananchi wanaweza kuendelea kuwa na kiasi cha fedha taslimu kwa matumizi ya dharura au pale mifumo ya kielektroniki inapokabiliwa na changamoto.

Kuhusu hatua za kisheria, Bi. Moses amesema, adhabu zipo kwa watu wanaoharibu fedha kwa makusudi ikiwemo adhabu ya kifungo, akisisitiza kuwa msisitizo wa Benki Kuu kwa sasa ni kuongeza elimu ili wananchi waelewe wajibu wao katika kutunza fedha.

Ameongeza kuwa, hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa pale inapobainika kuwa kuna ukiukwaji wa sheria, akieleza kuwa kutoa elimu hakumaanishi Benki Kuu haina uwezo wa kusimamia sheria na kuchukua hatua dhidi ya wahusika.

Bi. Moses amewataka waandishi wa habari kutumia nafasi zao kuelimisha umma kuhusu matumizi sahihi ya fedha, akisisitiza kuwa kulinda noti na sarafu ni jukumu la kila mwananchi na ni sehemu ya kulinda rasilimali za taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here