Rais Samia aagana na Balozi wa Afrika Kusini, azungumza na Mwekezaji kutoka Qatar

DAR ES SALAAM- Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo tarehe 06 Novemba, 2026, amekutana na kuzungumza na Balozi wa Jamhuri ya Afrika Kusini nchini, Mheshimiwa Noluthando Mayende-Malepe, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Balozi Mayende-Malepe, anayemaliza muda wake wa utumishi nchini, amemshukuru Rais Dkt. Samia, Serikali na wananchi wa Tanzania kwa ushirikiano na ukarimu aliopata katika kipindi chote alichohudumu nchini.

Amesema, Tanzania imekuwa na nafasi ya kipekee katika utumishi wake kutokana na ukarimu wa Watanzania na uhusiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya Tanzania na Afrika Kusini, ulioasisiwa wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.

“Tanzania ndiyo nchi niliyoifurahia zaidi kuhudumu katika kazi yangu ya ubalozi,” amesema Balozi Mayende-Malepe, akieleza kuwa anaondoka akiwa na kumbukumbu nzuri za maisha na utumishi wake nchini.

Aidha, Balozi Mayende-Malepe amepongeza mchango wa Tanzania katika masuala ya kikanda na kimataifa. Vilevile, ameyakaribisha makampuni zaidi ya Tanzania kufanya biashara na kuwekeza nchini Afrika Kusini.

Kwa upande wake, Rais Dkt. Samia amempongeza Balozi Mayende-Malepe kwa kuhitimisha utumishi wake nchini na kumshukuru kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini.
Amesema, biashara kati ya nchi hizo mbili imeongezeka katika kipindi cha utumishi wa Balozi Mayende-Malepe, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia fursa zilizopo kuongeza biashara na uwekezaji zaidi kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Balozi Mayende-Malepe amehudumu nchini kwa miaka minne tangu alipowasilisha Hati ya Utambulisho kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 25 Agosti, 2022.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amekutana na kuzungumza na Dkt. Khalid bin Mohammed bin Abdullah Al Attiyah, Mwenyekiti wa kampuni ya Thirty-Five Investment Holding ya Dola la Qatar.

Dkt. Al Attiyah ameeleza nia ya kampuni hiyo kuwekeza katika kilimo na ufugaji nchini. Fursa zilijadiliwa ni pamoja na uzalishaji wa sukari na ufugaji wa ng’ombe katika eneo la Kongwa, mkoani Dodoma.

Katika sekta ya uvuvi, mazungumzo yamehusu fursa za uvuvi wa bahari kuu na uwekezaji katika mitambo ya uchakataji na miundombinu ya kuhifadhi samaki katika Bandari ya Uvuvi Kilwa.
Halikadhalika, Dkt. Al Attiyah amesema kampuni yake inatathmini fursa za kuwekeza katika miundombinu ya usafiri Zanzibar, ambako tayari majadiliano yameanza kati ya timu yake na wataalamu kutoka taasisi husika kuhusu miradi inayopendekezwa.

Rais Dkt. Samia amezitaka taasisi zinazohusika kuendeleza majadiliano na kampuni hiyo kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni ili kubaini fursa zinazoweza kuendelezwa kwa manufaa ya pande zote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here