JKT yatangaza nafasi za mafunzo ya kujitolea kwa vijana mwaka 2026/27

NA DIRAMAKINI

JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza nafasi za kujiunga na mafunzo ya kijeshi kwa kujitolea kwa mwaka 2026/27, zinazolenga vijana kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wenye sifa na taaluma mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 12, 2026 katika Makao Makuu ya JKT jijini Dodoma, Mkuu wa Tawi la Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema, mchakato wa vijana kuomba nafasi hizo na kuchaguliwa utaratibiwa na Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanakoishi waombaji.

Amesema, nafasi hizo zimezingatia pia vijana wenye taaluma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), mifumo ya kompyuta na usalama wa mtandao, pamoja na wale wenye ujuzi wa ufundi na ufundi stadi (VETA).

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabena, vijana wenye stashahada (Diploma) katika fani za Teknolojia ya Habari, Mifumo ya Taarifa za Kibiashara, Sayansi ya Kompyuta, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), pamoja na Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Kihalifu wa Kidijitali, wanahimizwa kuomba nafasi hizo.

Aidha, vijana wenye shahada za Sayansi ya Kompyuta, Teknolojia ya Habari, Uhandisi wa Kompyuta, Teknolojia ya Habari za Kibiashara, Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Kihalifu wa Kidijitali, pamoja na Mitandao ya Kompyuta na Uhandisi wa Usalama wa Taarifa, wanakaribishwa kujitokeza.

Katika kundi la pili, JKT imewahimiza walimu wa mafunzo ya ufundi stadi (VETA) wenye utaalamu katika fani za uchomeleaji, ufundi magari, umeme wa magari, ufundi bomba, upakaji rangi, uashi, TEHAMA, ubunifu wa mavazi, ukarani, useremala, ushonaji, pamoja na ufundi wa majokofu na viyoyozi, kutumia fursa hiyo kupitia mikoa yao.

Amesema, usaili wa vijana wanaoomba kujiunga na mafunzo hayo utaanza Novemba 16, 2026, katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Vijana watakaofanikiwa kuchaguliwa wanatakiwa kuripoti katika makambi ya JKT kuanzia Desemba 10 hadi 15, 2026.

Katika hatua nyingine, Brigedia Jenerali Mabena amesisitiza kuwa vijana wanaopata nafasi za mafunzo hayo wanapaswa kuelewa kuwa JKT haitoi ajira wala haiwajibiki kuwatafutia ajira katika asasi, vyombo vya ulinzi na usalama au mashirika ya Serikali na yasiyo ya Serikali.

Badala yake, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea vijana nidhamu, ujuzi na uwezo utakaowawezesha kujitegemea na kujiajiri baada ya kukamilisha mkataba wao wa mafunzo.

Ameeleza kuwa, sifa za waombaji pamoja na maelekezo kuhusu vifaa wanavyopaswa kwenda navyo wakati wa kuripoti kambini vinapatikana kupitia tovuti rasmi ya Jeshi la Kujenga Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here