Tanzania yaunga mkono maazimio ya SADC kukabiliana na Maafa ya El Niño

DODOMA- Serikali ya Tanzania imeunga mkono maazimio sita ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), yanayolenga kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa katika ukanda huo, hususan kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño.
Msimamo huo umetolewa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Kaspar Mmuya, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ambapo aliwasilisha msimamo wa Tanzania katika Mkutano wa Saba wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri.

Ni wenye dhamana ya Usimamizi wa Maafa katika nchi wanachama wa SADC, uliofanyika kwa njia ya mtandao leo, Novemba 12, 2026 jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

Mmuya amesema, Tanzania inatambua na kupongeza jitihada zinazofanywa na nchi wanachama pamoja na Sekretarieti ya SADC katika kujiandaa kukabiliana na maafa yanayoweza kujitokeza kutokana na El Niño, ikiwemo kuandaa mipango ya dharura ya kitaifa na kikanda kwa lengo la kupunguza madhara.
Amesema, jitihada hizo ni pamoja na kuratibu mazoezi ya utayari wa kukabiliana na vimbunga na mafuriko kupitia Timu ya Kikanda ya Utayari wa Kukabiliana na Dharura, yaliyofanyika Nacala, Msumbiji, pamoja na maandalizi ya taarifa ya kikanda kuhusu hali ya usalama wa chakula na lishe kwa mwaka 2026.

“Tanzania inaunga mkono na kuridhia maazimio yote kuanzia Uamuzi Na. 1 hadi Na. 6 kama yalivyopendekezwa na Sekretarieti,” amesema.

Ameongeza kuwa Sekretarieti imeendelea kuratibu usambazaji wa taarifa za utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za mapema, kuandaa mkakati wa kikanda wa kuhifadhi vifaa vya akiba kwa ajili ya misaada ya kibinadamu na mwongozo wa utekelezaji wa hatua za mapema za kupunguza athari za vihatarishi mbalimbali kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030.
Akisisitiza maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele, Mmuya amesema ni muhimu nchi wanachama kuimarisha usalama wa chakula na lishe kwa kuhakikisha taarifa zinazohusu eneo hilo zinaandaliwa na kuwasilishwa kwa wakati.

Amesema, upatikanaji wa chakula cha kutosha, salama na chenye virutubisho muhimu ni sehemu muhimu ya usimamizi wa maafa kwa kuwa unasaidia kulinda maisha ya wananchi, kupunguza athari za majanga na kuimarisha ustahimilivu wa jamii.

"Sekretarieti ya SADC kushirikiana na washirika wa maendeleo kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali fedha na utaalamu utakaowezesha kuimarisha utayari wa kikanda, kutekeleza hatua za mapema na kutoa misaada ya kibinadamu kwa haraka wakati wa maafa,"amesema.
Pia, amesisitiza umuhimu wa utaratibu wa kikanda wa kuhifadhi vifaa vya dharura kuzingatia vihatarishi vya majanga, haki na usawa, uendelevu wa kifedha, uwazi na kuimarisha mifumo ya kitaifa iliyopo.

Kwa upande mwingine, Mmuya ameipongeza Sekretarieti ya SADC kwa kuendelea kutekeleza ajenda ya kuimarisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura (SHOC), ikiwemo kuimarisha timu ya utayari wa kukabiliana na dharura kupitia mafunzo, mazoezi na upatikanaji wa vifaa.

Amesema, hatua hizo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa nchi wanachama kukabiliana na maafa, kupunguza madhara kwa wananchi na kulinda maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika ukanda wa SADC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here