ZANZIBAR- Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Oman (JPC) ni fursa muhimu ya kuharakisha utekelezaji wa makubaliano na kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo kati ya nchi hizo mbili.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Novemba 10, 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mhe. Sayyid Badr bin Hamad bin Hamood Albusaidi, na kusisitiza umuhimu wa kutumia uhusiano wa kihistoria na kindugu kati ya Zanzibar na Oman kukuza fursa za kiuchumi, hususan katika Uchumi wa Buluu, utalii, uvuvi na ufugaji wa samaki.
Aidha, ameishukuru Serikali ya Oman kwa mchango wake katika sekta za elimu, maji na uhifadhi wa urithi wa kihistoria Zanzibar, huku akiwakaribisha wawekezaji wa Oman kutumia fursa zilizopo Zanzibar.
Kwa upande wake, Mhe. Albusaidi amesema Oman itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania, akieleza kuwa kuna fursa kubwa ya kuongeza biashara, uwekezaji na utalii kati ya nchi hizo mbili.
Katika mazungumzo hayo walikuwepo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo; Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Maulidah Bwanakheir Hassan; Balozi wa Oman nchini Tanzania, Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shaidani; na Balozi Mdogo wa Oman Zanzibar, Mhe. Said Salim Hamed Al Sinawi, pamoja na viongozi wengine.
Tags
Biashara na Uwekezaji
Dkt. Hussein Ali Mwinyi
Habari
Kimataifa
Oman
Rais Hussein Mwinyi
Zanzibar











