Utata waibuka kifo cha mlinzi wa Makamu wa Rais

NAIROBI, Utata unaozingira kifo cha Sajini Kipyegon Kenei, aliyekuwa Mkuu wa Usalama katika Ofisi ya Makamu wa Rais wa Kenya,William Ruto unaendelea kuzua maswali mengi kuliko majibu baada ya idara inayochunguza uhalifu (DCI) kudai kwamba, kuuawa kwa ofisa huyo kunahusiana na matukio katika ofisi ya kiongozi huyo. 

Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi, Goerge Kinoti amesema kwamba, Sajini Kemei aliuawa kikatili, kinyume na habari za awali kwamba alijiua mwenyewe. 

Mwili wa Kenei ulipatikana nyumbani kwake wiki mbili zilizopita ukiwa na jeraha la risasi. Kulingana na taarifa ya polisi, marehemu alijiua. 

Kifo cha askari huyo kilitokea wakati ambapo alitakiwa kuandika taarifa ya maelezo kwa polisi kuhusu washukiwa wa sakata la zabuni hewa ya ununuzi wa silaha za mamilioni ya pesa walipotembelea ofisi ya Ruto jijini Nairobi.
Kifo chake kimezua mjadala mkali nchini Kenya huku baadhi ya watu wakisema, huenda mlinzi huyo aliuawa mahali tofauti na mwili wake ukapelekwa nyumbani kwake kwa lengo la kuficha ukweli juu ya uhalisi wa kilichomuua. 

Kabla ya mwili wa afisa huyo kupatikana, ofisi ya Ruto ilikuwa imetoa taarifa ikisema kwamba alikuwa ametoweka. 

Mbali na kutilia shaka maelezo ya polisi, Wakenya mitandaoni hawakuridhishwa na hatua ambazo ofisi ya Ruto ilichukua pale Kenei alipokosa kufika kazini badaye na kujiwasilisha kwa wapelelezi kuandikisha taarifa. 

Zabuni hewa ya silaha yalipuka 

Mkuu wa DCI, George Kinoti, alisema awali kwamba, Kenei alitakiwa kuandikisha taarifa kwa polisi kueleza jinsi aliyekuwa Waziri wa Michezo, Rashid Echesa na washukiwa wengine wanne walivyowaingiza raia wa kigeni katika ofisi ya Ruto, na hata kutia sahihi kandarasi feki ya kuiuzia Wizara ya Ulinzi silaha. 

Kwa mujibu wa Kinoti ambaye alionyesha wanahabari picha zilizochukuliwa na kamera za siri yaani CCTV, Kenei anaonekana akiwafungulia mlango na kuwaelekeza Echesa na ujumbe wake katika ofisi ya Naibu Rais. 

Echesa, mwandani wa karibu wa Ruto, ameshtakiwa kwa kujaribu kujipatia dola za Marekani 395, 442,000 kutoka kwa wafanyabiashara wa Poland kwa kuwaahidi zabuni ya kuiuzia idara ya ulinzi ya Kenya vifaa vya kijeshi. 

Ruto ajitetea vikali 

Ruto ameshutumiwa sana kufuatia kesi hiyo, huku viongozi wengine wakihoji vipi ulaghai wa hali ya juu unaweza kufanyika katika ofisi yake bila yeye kujua. Kwa upande mwingine, naibu huyo wa rais ameshutumu ripoti hizo kama porojo zenye hila. 

Ruto amejitetea vikali kwamba hakukutana na waziri huyo wa zamani wa michezo, Echesa pamoja na wafanyabiashara wake waliotembelea ofisi yake na hakuhusika katika mkataba huo bandia uliodaiwa kugharimu dola milioni 397. 

Ingawa inaonekana kifo cha aliyekuwa mkuu wa usalama katika Ofisi ya Naibu Rais wa Kenya kinachukua mkondo wa kisiasa, wengi wanafuatilia sakata hiyo kwa umakini mkubwa wakitarajia kwamba ukweli utapatikana.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news