Mgombea NCCR Mageuzi Joyce Sokombi apangua propaganda Musoma Mjini asema ushindi ni asubuhi sana

MGOMBEA Ubunge kupitia Chama cha NCCR Mageuzi Jimbo la Musoma Mjini,Joyce Sokombi amewataka wanachama wa chama hicho na wananchi kwa  ujumla, kuzipuuza propaganda zinazoenezwa dhidi yake kuwa, amejiondoa kwenye  mbio za kuwania ubunge wa jimbo hilo,anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.

Ameyasema hayo muda mfupi akiwa katika mwendelezo wa kampeni za kunadi sera na kuomba kura kwa wananchi wa eneo la Zanzibar Kata ya Makoko Manispaa ya  Musoma katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

"Puuzeni uzushi unaoenezwa na baadhi ya watu kwamba nimejiondoa kuwania ubunge, sijajiondoa na sitojiondoa kabisa, dhamira yangu ni kutimiza ndoto yangu ya  kuwakomboa wananchi wa Musoma Mjini  baada ya ninyi  kunichagua Oktoba 28,mwaka huu, najua changamoto za wananchi wa Zanzibar  ni  ukosefu wa shule eneo hili naahidi kuwezesha ujenzi wanafunzi wasitembee umbali mrefu, pamoja na kushughulikia tatizo la barabara za mitaa na huduma ya maji safi na salama eneo hili la Zanzibar,"amesema Sokombi. 

Sokombi pia amebainisha kwamba, anashauku kubwa ya kuona kero zinazowakabili wazee na makundi maalumu anazitatua iwapo atachaguliwa kwa kuanzisha programu maalumu ya kutembelea kata kwa kata kuratibu na kushughulikia kero zao kusudi azipatie ufumbuzi.

Ashura Paul na Hilda Juma Wakazi wa Zanzibar kata ya Makoko wakizungumza na Diramakini wamesema watafurahi endapo Sokombi atashinda na kuweza kutekeleza ahadi ya kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika eneo la Zanzibar kwani muda mwingi wamekuwa wakitumia kutafuta maji hivyo wataondokana na adha hiyo.

No comments

Powered by Blogger.