Dkt.Mwinyi kuwashughulikia watendaji wanaopunja wakulima wa karafuu, aahidi fursa za ajira, afya,maji

Mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameendelea na kampeni za kunadi sera, ilani kwa wananchi visiwani Pemba huku akiwaomba wananchi wampe ridhaa ili akatekeleze kwa vitendo yaliyomo ndani ya ilani na vipaumbele vyake,anaripoti Mwandishi Diramakini.
Katika kampeni zake amewaahidi wakulima wa zao la karafuu kisiwani Pemba kuwa, pindi akipata ridhaa atahakikisha zao hilo linaongezeka thamani ili kuwanufaisha wote na kuongeza pato la taifa.
Pia ameahidi miundombinu bora ikiwemo kujenga viwanda vitakavyozalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao hilo hapa nchini badala ya kuuza nchi za nje pekee.
Ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wakulima wa zao la karafuu, chumvi na viungo nje kidogo ya mji wa Chake Chake kisiwani Pemba.
Dkt.Mwinyi amesema kwamba, ana nia ya dhati ya kuyafanya hayo kwa vitendo.

Pia amesema, zao hilo litawekewa mazingira bora ili wananchi wapate fedha nyingi na serikali itakuwa na pato ambalo litasaidia kuimarisha huduma za kijamii zikiwemo sekta ya afya, elimu,uvuvi,maji safi na salama, miundombinu ya barabara na umeme na kilimo.

Dkt. Mwinyi amesema,akipata ridhaa ya kuongoza Zanzibar atapambana na baadhi ya watendaji wa Shirika la Biashara Zanzibar wanaotuhumiwa kuwapunja wakulima pindi wanapopima karafuu zao katika mizani hivyo kupewa fedha ndogo kuliko karafuu wanazopima kisiwani humo.
Dkt.Mwinyi amesema,alichukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo, ili kuwatumikia wananchi wote wakiwemo wakulima hao waweze wafaidike na jasho lao.

Pia mesema, kwa sababu ana nia ya kuimarisha uwajibikaji, ndio maana kama watendaji hao hawataki kubadilika, atawawajibisha kisheria ili kila mmoja aonyeshe ufanisi katika nafasi yake.

Dkt.Mwinyi akizungumzia kuhusu mikopo kwa wakulima wa zao hilo kwa ajili ya kushughulikia mashamba yao, amewahidi kuwa hilo linawezekana na anaamini hatua hiyo inaweza kuongeza tani za uvunaji wa zao la karafuu ili kutosheleza mahitaji ya ndani na nje.

Aidha,kuhusu wakulima wa viungo na wale wazalishaji wa chumvi kisiwani Pemba, amewahidi kuwapatia mitaji na mikopo yenye masharti nafuu waweze kuzalisha kwa wingi.

Dkt.Mwinyi amesema, haiwezekani mkulima wa iliki, chumvi au vanilla kutakiwa kupeleka waraka wa nyumba kama ithibati ya kupewa mkopo.

“Mkinichagua kuwa Rais wa Zanzibar, nitazungumza na mabenki kuona wanapunguza masharti ya mikopo au wakati mwingine Serikali kuwa ndio dhamana, ili nao wapate kujiendeleza,’’amefafanua Dkt.Mwinyi.

Amesema pia atahakikisha anaweka mazingira imara zaidi kwa wakulima hao, ikiwa ni pamoja na kuangalia upya suala la bei ili waendelee kunufaika.

Amesema, hadi mwaka 2018 kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 iliyosimamiwa na Rais wa Awamu ya Saba, Dkt. Ali Mohamed Shein, kulikuwa kunazalishwa tani 8,277 ambapo kama akipata ridhaa atahakikisha kuna ongezeko la uzalishaji hadi kufikia tani 10,000 kwa mwaka.

Mgombea huyo ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane ijayo, atakayongoza, itaendelea kuimarisha hali za kipato cha wakulima wa zao la karafuu na kuanza kuchakata mafuta ya majani ya karafuu.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdulla Juma Mabodi alisema, Dkt. Hussein ni mchapakazi hodari na ndio maana kwa nafasi yake ya Waziri wa Ulinzi bado nchi ipo salama.

Mabodi amesema,Dkt.Mwinyi ana sifa zote za kuwa Rais wa Zanzibar na hasa kwa vile amekuwa akiyapenda makundi kama ya wakulima wa zao la karafuu, mwani, viungo na hata wanaozalisha chumvi visiwani humo.

No comments

Powered by Blogger.