Kamati yafunguka adhabu dhidi ya CHADEMA Ubungo

Kamati ya Maadili ya Jimbo la Ubungo jijini Dar es salaam imesema kuwa adhabu iliyotolewa dhidi ya mgombea Ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni sahihi kwa mujibu wa Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2020 na si shinikizo toka kwa mtu, anaripoti Rachel Balama (Diramakini) Dar es Salaam.

Septemba 23, mwaka huu kamati hiyo ilikaa kikao na kutoa adhabu ya kusitisha kampeni kwa muda wa siku saba kwa mgombea huyo kutokana na kukiuka Maadili ya Uchaguzi.

Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya wajumbe wamesema kuwa, kamati hiyo ambayo inaundwa na wajumbe kutoka vyama vilivyosimamisha wagombea wa ubunge ipo kwa mujibu wa sheria na inafanya kazi pasipo kuingiliwa na mtu yoyote kwa maslahi yake binafsi na kwamba maamuzi yanayotolewa yanatakiwa yatekelezwe na si vinginevyo.

Kwa upande wake Mjumbe kutoka Chama cha Demokrasia Makini, Leonard Monalinze amesema, adhabu hiyo ilitolewa na kamati hiyo kwa kuzingatia ushahidi kutoka pande zote mbili yaani mlalamikaji na mlalamikiwa.

"Hakuna mtu yoyote ambaye ameshinikiza adhabu hiyo dhidi ya Boniface Jacob haya ni maamuzi ya wajumbe wote wa kamati baada ya kusikiliza shauri hilo, wajumbe tulipiga kura za siri na ndizo ziliziamua matokeo ya adhabu hiyo tofauti na taarifa za kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinasambazwa zikieleza kwamba Msimamizi ndio alitoa adhabu hiyo kitu ambacho si sahihi,"amesema.

Naye  Mjumbe kutoka Chama cha Kijamii cha CCK, Innocent Shirima amesema kuwa,suala hilo lilipokuwa linasikilizwa Mjumbe kutoka Chadema naye alikuwa ni miongoni mwao.

Kampeni za mgombea huyo wa Chadema zimesitishwa kutokana na mgombea wa Chama cha CCK, Emma Mwakisole pamoja na mgombea wa Ada Tadea kupeleka malalamiko kwenye kamati kwamba Jacob alikiuka maadili ya uchaguzi kwa kuzidisha muda wa kampeni jambo ambalo ni kinyume na maadili.

Aidha,wajumbe hao walivitaka vyama vinavyoshiriki uchaguzi kuhakikisha vinaeshimu maadili ya uchaguzi ambayo yalipitishwa na vyama vyote vya siasa hapa nchini.

Wajumbe hao wamesema hawatasita kuwachukulia hatua wagombea wote ambao watathibitika kukiukaa kanuni za maadili ya uchaguzi ili mwisho wa siku uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu.

Kamati hiyo ya Maadili ya Jimbo inaundwa na mjumbe mmoja mmoja kutoka katika Chama cha NRA, CCM, Chadema, Demokrasia Makini, ACT wazalendo , ADC, UMD CCK, SAU, Ada Tadea, Chauma na, TLP.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news