Mwanga wa mafanikio kwa Iringa mpya umeanza kuangaza, ni baada ya Septemba 28, 2020 katika Uwanja wa CCM Samora mkoani Iringa, wana Iringa wenyewe kumuonyesha Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli kuwa, wapo tayari kwa mabadiliko, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mabadiliko hayo wamekiri mbele ya mkuu huyo wa nchi kuwa, ndiyo yatakayowawezesha kuifanya Iringa kuwa mpya ikiwa ni baada ya Jimbo la Iringa Mjini kuwa chini ya upinzani kwa muda mrefu.
Dkt.Magufuli ameyasema hayo mbele ya umati wa maelfu kwa maelfu ya wananchi waliofurika ndani na nje ya Uwanja wa CCM Samora wakati akinadi sera na ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.
Huo ni ushaidi tosha kwamba, kwa wananchi ambao wanakusanyika katika mikutano ya kampeni wanatamani kufahamu kwa kina ni mambo gani wagombea iwapo watapata ridhaa watakuja kuwatendea, wakati Dkt.Magufuli akitekeleza hilo kwa umakini mkubwa, baadhi ya wagombea wengine wameendelea kutumia muda mwingi kufanya mashambulizi binafsi kati ya mtu na mtu ama taasisi, jambo ambalo limekuwa likichukua muda mwingi na pengine kuwafanya wananchi ambao wanataka kujua jambo kutoka kwao kujikuta wanachoka na kuondoka katika mikutano.
Tuyaache hayo, tuendelee na Dkt.Magufuli ambaye leo Septemba 28, 2020 ametimiza mikoa 11 katika kampeni zake ambazo zimejikita kuwaelezea wananchi waliyokusudia kuja kuwafanyia tena iwapo watawapa ridhaa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Dkt.Magufuli amesema, yeye ni Rais wa Watanzania, wala haoni shida kwa mtu yeyote ambaye atakuwa anambeza kwa sababu ya kutosafiri kwenda nje ya nchi, kwani kuwafikia Watanzania tena wanyonge ndiyo faraja yake.
“Mimi lazima niwe mtumishi wa wanyonge,mtumishi wa watu na ndio maana siku zote nimekuwa barabarani kutatua kero za wananchi,”amesema Dkt.Magufuli.
Dkt.Magufuli amesema, Ilani ya Uchaguzi 2020-2025, imezungumzia kwa kina juu ya namna ya kuendeleza juhudi za kujenga taifa linalojitegemea kiuchumi kwa kutumia rasilimali mbalimbali zilizopo hapa nchini.
Amesema, rasilimali hizo nii pamoja na watu ,ardhi,madini,gesi asilia,misitu,wanyama,kutoka majini,bahari na nyinginezo nyingi. Dkt.Magufuli amebainisha, kutokana na uongozi imara watahakikisha rasilimali hizo zinazidi kuwa baraka kwa Watanzania wote ikiwemo kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
“Ndugu zangu, siku zote nazungumza Tanzania ni tajiri na ina mambo mengi na haya yote yapo katika ilani yetu ya chama sura ya kwanza na ya pili,”amesema Dkt.Magufuli huku akiongeza kuwa, ilani yao imeeleza mipango na mikakati iliyopangwa kutekelezwa ndani ya miaka mitano ijayo kwa manufaa ya Taifa na Watanzania wote.
“Hii ilani ndio mkataba wa Serikali itakayoingia madarakani na wananchi,ambapo pia tunatakiwa kutengeneza ajira milioni nane ambapo miaka mitano iliyopita ajira zilizotengenezwa zilikuwa milioni sita,”amefafanua Mgombea Urais huyo.
Dkt.Magufuli amesema, ajira hizo zimetokana na kuwepo zahanati 1198,Vituo vya afya 487,ununuaji wa ndege 11 ambapo nane zimefika tayari,ukarabati wa barabara zaidi ya kilomita 300,utengenezaji wa reli ya kisasa ya umeme zaidi ya ajira 10,000, Bwawa la Mwalimu Nyerere zaidi ya ajira 10,000 zimetengenezwa ambapo wapo wanaojenga,wanaouza vyakula,wanaofanya kazi na wakandarasi pamoja na watumishi mbalimbali wa maeneo hayo.
“Tunataka kipindi cha miaka mitano mingine tutengeneze ajira zaidi ya milioni nane na huo ndio uchumi wa kati kuliko uchumi wa mwanzo wa kimasikini,ili kufikia malengo haya tutaboresha mazingira ya uchumi na biashara kwa kuendelea kufanya mageuzi katika sheria na kanuni,Kodi,tozo na utendaji wa sekta ya umma kwa kuzingatia muongozo wa uboreshaji wa mazingira nchini,”amesema.
Amesema,
Ilani ya chama chao ya uchaguzi inaeleza misingi au nguzo muhimu za
Serikali ya CCM, endapo itachaguliwa itaendelea kusimamia ikiwemo
kulinda uhuru wa nchi,kudumisha amani,umoja,mshikamano na Mapinduzi ya
Zanzibar pamoja na Muungano.
Amesema, uchaguzi huu ni muhimu
kuendelea na mageuzi ya sasa na kupata viongozi watakaobeba maendeleo ya
nchi huku akiwasisitiza kuwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndio chama
kinachoweza kuleta maendeleo kwa kasi kubwa.
Wakati huo huo
amesema, miaka mitano ijayo Serikali inatarajia kufanya mageuzi makubwa
ya kiuchumi mkoani Iringa ambayo yatakuwa ni mwendelezo wa yale
yaliyofanyika awali.
Miongoni mwa mafanikio ya awali ni pamoja na
upanuzi wa chumba cha wagonjwa mahututi,kujenga jengo la wagonjwa wa
dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Upanuzi wa Hospitali ya Wilaya
Manispaa ya Iringa na kujernga hospitaliu tatu mpya. Pia amesema
wamefanya upanuzi wa vituo vya afya vitano ambapo viwili vinaendelea
kujengwa na zahanati 23.
“Tumeleta kiasi cha shilingi Bilioni
33.74 katika elimu kwa ajili ya elimu bila malipo kwa watoto hapa
Iringa, upanuzi Chuo Kikuu Mkwawa,kukarabati Chuo cha Walimu,Chuo cha
Maendeleo ya Wananchi Ilula na Shule ya Ufundi Ifunda,Tosamanganga, pia
tumejenga mabweni,madarasa na vyuo vya ufundi,kwa upande wa maji
Serikali imetekeleza miradi ya maji 43 yenye thamani ya sh.bilioni 20.3
na miradi 79 inaendelea kwa gharama ya sh.bilioni 22.94,”amesema.
Mbali
na hayo amesema,upatikanaji wa maji vijijini katika Mkoa wa Iringa
umefikia asilimia 72 kutoka asilimia 60 hadi 66,kuhusu umeme wamefikisha
umeme katika vijiji 242 ambapo vijiji 37 ndio vilivyobaki katika
kuwashwa umeme na vinatarajiwa kupata nishati hiyo mapema.
Dkt.Magufuli
amesema kwa upande wa miundombinu wamekarabati barabara ya Mafinga
zaidi ya kilomita 74.1 pamoja na kupanga kuupanua uwanja wa ndege Nduli
ili kuwa mkubwa na kufanya Mkoa wa Iringa kuwa kitovu cha utalii katika
Nyanda za Juu Kusini huku akisisitiza kuwa, wakipewa ridhaa kuna mambo
mengi zaidi ya hayo watayatekeleza ikiwemo kuboresha, kuanzisha na
kuimarisha sekta ya utalii ili ifungue fursa nyingi za ajira.