Simba SC, Azam FC, Polisi Tanzania FC zachekelea ushindi

Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, umezidi kuwapa raha mashabiki wa Klabu ya Simba SC baada ya leo Septemba 26,2020 kujinyakulia ushindi mnono,anaripoti Mwandishi Diramakini.

Ushindi huo ambao ni mwendelezo wa matokeo ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara umepatikana baada ya Simba SC kuicharaza Gwambina FC mabao matatu kwa sufuri.

Matokeo ya leo yanaifanya Simba SC kufikisha alama 10 baada ya kucheza mechi nne huku ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Azam FC inayoongoza kwa alama 12 hadi sasa.

Simba SC kipindi cha kwanza imepumzika ikiwa inaongoza moja kwa sufuri kupitia kwa bao la mshambuliaji wa Kimataifa Meddie Kagere 39' akimalizia pasi ya kiungo kutoka Msumbiji, Luis Miquissone.

Aidha, dakika tano baada ya kuanza kipindi cha pili,Serge Pascal Wawa akaifungia Simba SC bao la pili kwa shuti la mpira wa adhabu, baada ya kiungo mpya, Rally Bwalya kuangushwa umbali wa mita 30 uwanjani hapo.

Pia mshambuliaji mpya,Chris Mutshimba Kopa Mugalu aliyekuchukua nafasi ya Kagere kipindi cha pili, akaifungia Simba SC bao la tatu 90' akimalizia pasi ya mtokea benchi mwenzake,Bernard Morrison.
LIVE SIMBA SC VS GWAMBINA FC

 
Gwambina ya mkoani Mwanza iliyopanda Ligi Kuu msimu huu inakamilisha mechi nne bila ushindi, ikifungwa tatu na kutoa sare moja.

Awali Azam FC ilirejea kileleni baada ya ushindi wa moja kwa sufuri dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons, bao la Prince Mpumeled Dube 90' Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa lilitosha kufunga hesabu.

Wakati huo huo,Polisi Tanzania imeibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC, mabao ya Marcel Kaheza 11' na 61' na Tariq Seif 33' Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Ligi Kuu itaendelea kesho kwa Ruvu Shooting kuwa wenyeji wa Biashara United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Mwadui FC na Ihefu Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga na Mtibwa Sugar na Yanga SC Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro huku hatua ya nne ikitarajiwa kukamilika Jumatatu kwa mchezo mmoja tu, Coastal Union wakiwa wenyeji wa JKT Tanzania katika Uwanja wa Mkwakwani,Tanga.

No comments

Powered by Blogger.