Simba SC waduwazwa, Dodoma Jiji FC, KMC wachekelea

PENGINE leo unaweza kusema haikuwa kazi rahisi katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwani mabingwa wa Ligi Kuu Simba SC wamelazimishwa kwenda sawa na Mtigwa Sugar, anaripoti MWANDISHI WETU kutoka DIRAMAKINI.

Mchezo huo ambao Simba SC walianza kuzifumania nyavu za Mtibwa Sugar kipindi cha kwanza kwa bao lililofungwa na Mzamiru Yassin 45', Mtibwa Sugar walipindua meza kupitia Boban Zirintusa 46'. Matokeo ambayo yaliendelea hadi dakika za mwisho timu hizo zikatoka kwa mfanano wa goli.
 
Simba SC inayofundishwa na Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck inarekodi sare ya kwanza katika mchezo wa pili tangu msimu wa Ligi Kuu uanze mapema mwezi huu.

Awali ilishinda 2-1 ugenini dhidi ya wageni katika Ligi Kuu, Ihefu FC katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Wakati huo huo,Mtibwa Sugar ambayo inanolewa na mwalimu Zubery Katwila huu unakuwa ni mwanzo ambao si bora zaidi kutokana na matokeo ya awali ambapo walizungusha 0-0 na Ruvu Shooting, kupitia kabumbu safi lililotandazwa Uwanja wa CCM Gairo mkoani Morogoro.

Mbali na mtanage huo, huko Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, wenyeji Dodoma Jiji FC imeichapa JKT Tanzania 2-0, mabao ya Jamal Mtegeta 50' na Dickson Ambundo 80'.

Wakati huo huo KMC imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mabao ya KMC yamefungwa na Hassan Kabunda 21' na Kenneth Masumbuko 85', wakati la Prisons limefungwa na Kassim Mdoe 39'.Habari mpya soma hapa.

Septemba 13, 2020 Ihefu itawakaribisha Ruvu Shooting kuanzia saa 8:00 mchana katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Biashara United na Mwadui FC kuanzia saa 10:00 jioni Uwanja wa Karume Musoma mkoani Mara na baadaye saa 1:00 usiku,Yanga SC watakutana na Mbeya City Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Pia Septemba 14, 2020 kutakuwa na mchezo mmoja tu wa kukamilisha awamu ya pili, Namungo FC wakiwaalika Polisi Tanzania kuanzia saa 10:00 jioni Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa mjini Lindi.

No comments

Powered by Blogger.