Msajili awaita viongozi wa vyama vya siasa, NEC yatoa msisitizo tena

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania imewaita viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa nchini humo ili wazungumzie utekelezaji wa sheria zinazosimamiwa na ofisi hiyo, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Taarifa ya ofisi hiyo kwa Makatibu Wakuu wa Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu, imeeleza kuwa kikao hicho cha viongozi wakuu wa vyama na Msajili wa Vyama vya Siasa kitafanyika Oktoba 2, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Naibu Msajili wa Vyama Vya Siasa, Sisty Nyahoza kupitia taarifa hiyo ameeleza kuwa, kikao hicho kitaanza saa mbili asubuhi na kitaanza mapema kwa kuwa Ijumaa ni siku ya ibada.

“Washiriki watakuwa ni Mwenyekiti wa Taifa na Katibu Mkuu, mnaombwa kuhudhuria bila kukosa,”imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa kwa niaba ya Msajili wa Vyama Vya Siasa.

Mbali na hayo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo udiwani, ubunge na urais kuzingatia maadili ya uchaguzi katika kipindi cha kampeni zao ikiwemo kuepuka lugha za kashfa na uchochezi ambavyo ni viashiria vya uvunjifu wa amani iliyopo katika Taifa.

Wito huo umetolewa na Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Mbarouk Mbarouk wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi jijini Dodoma.

Amesema, kunapotokea malalamiko yoyote ya kimaadili hatua stahiki zichukuliwe ikiwemo kuwasilisha malalamiko kwenye kamati za maadili ndani ya muda uliowekwa.

Pia amesema,tume inaendelea kusimamia na kuendesha uchaguzi kwa kutumia sheria za uchaguzi, hivyo vyama vya siasa,wagombea na wananchi wanakumbushwa kuwa katika kipindi hiki sheria nyingine za nchi hazijasimama.

"Kila mmoja anapaswa kujihadhari na vitendo ama matamshi ambayo husababisha vurugu kwa kisingizio cha uchaguzi,"amesema Jaji Mbarouk.

Pia amesema,NEC imejipanga kusimamia uchaguzi wa mwaka huu kwa kufuata katiba, sheria,kanuni na miongozo mbalimbali na inaamini kuwa kila mdau akitimiza wajibu wake kwa kufuata taratibu watanzania wataweza kupiga kura kwa amani siku ya Jumatano ya Oktoba 28, mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news