TAKUKURU yarejesha mamilioni ya fedha kwa wakulima wa miwa

"Mnamo tarehe 22 mwezi wa 11, 2019 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mvomero ilipokea taarifa ya malalamiko toka kwa wakulima wa miwa ambao ni wanachama wa Mtibwa Outgrowers Association (MOA) na Turiani Cane Outgrowers and Other Crops Primary Cooperative Society (TUCOCPRCOS LTD) wakilalamikia vyama hivyo kwa kutokulipwa madai yao ya fedha zaidi ya shilingi milioni 101,989,494.46 kwa wanachama wa MOA.

"Na shilingi milioni 116,618,247.00 kwa wanachama wa Chama cha TUCOCPRCOS LTD ambazo ni mauzo ya miwa yao iliyouzwa kwa kiwanda cha Sukari Mtibwa (Mtibwa Sugar Estates-MSE) kilichopo Turiani wilayani Mvomero kwa msimu wa mwaka 2015/2016.

"TAKUKURU ilishughulikia taarifa hiyo ambapo ilibainika kuwa, Kiwanda cha Sukari Mtibwa kilikwisha kuwalipa madai yote ya wakulima hao kwa msimu wa mwaka 2015/2016.

"Ilibainika pia kuwa fedha ambazo zilikusudiwa kuwalipa wakulima hao baada ya kupokelewa katika vyama vyao zilitumika kwa matumizi mengine ya vyama ikiwemo ununuzi wa kiwanja chenye ekari tatu mali ya chama cha TUCOCPRCOS LTD, ulipaji wa madeni kwenye taasisi za kifedha ambapo vyama vilikopa, pamoja na uendeshaji wa vyama kinyume na malengo yaliyokusudiwa kwa fedha hizo.

"TAKUKURU kama chombo cha mapambano dhidi ya rushwa inalo jukumu la kuhakikisha kuwa, fedha za wakulima wanyonge zinarejeshwa na kulipwa kwa kuwa ni haki yao. Kwa kuzingatia hilo, mnamo tarehe 11 mwezi wa 6, 2020 TAKUKURU ilifanya zoezi la kurejesha fedha jumla ya shilingi milioni 23,800,000.00 ambapo wanachama 62 wa TUCOCPRCOS LTD walirejeshewa kiasi cha shilingi milioni 15,800,000.00.

"Kwa kuwa TAKUKURU imedhamiria kuhakikisha kuwa fedha zote za wakulima wanyonge zinarejeshwa leo tena (Septemba 10, 2020) fedha nyingine kiasi cha shilingi milioni 20,000,000.00 ambazo ni shilingi milioni 10,000,000 kwa kila chama zitalipwa kwa wakulima 81 waliohakikiwa kwa utaratibu mzuri ulioandaliwa na TAKUKURU.

"Wakati huo huo TAKUKURU inaendelea kukamilisha mchakato wa zoezi hili ili kumuhudumia kila mwanachama anayestahili kulipwa matunda ya jasho lake.Ili kurahisisha zoezi hili, TAKUKURU inatarajia ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wanachama wa vyama hivyo.

"Rai yetu ni kuwa wanachama wenye madai wanatakiwa kufika kwa haraka kwenye ofisi za vyama vyao kwa ajili ya uhakiki mapema iwezekanavyo kulingana na utaratibu uliowekwa na TAKUKURU, pia wananchi wote wenye madai ya aina hiyo katika Mkoa wa Morogoro wanatakiwa kutoa taarifa kwa TAKUKURU ili washughulikiwe.

"Msisitizo mkubwa unatolewa kwa wote wenye dhamana katika vyama vya ushirika, SACCOS na AMCOS mkoani Morogoro kuwa waadilifu na kuhakikisha usimamizi mzuri wa fedha za wanachama wanyonge ili wanachama hao wafaidike na kazi za mikono yao,"hayo yamefafanuliwa kwa kina na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Janeth Machulya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news