TANESCO: TUNAUZA UMEME USIOKATIKA KWA GGML

SHIRIKA la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco) limesema linatauza umeme katika Mgodi wa Uchimbaji wa Dhahabu wa Geita (GGML) wenye ubora,unaokidhi mahitaji ya mgodi huo na usiokatika, anaripoti ROBERT KALOKOLA kutoka GEITA.

Mtambo wa umeme katika kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Mpomvu Mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Dkt.Alexander Kyaruzi leo wakati akikagua mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Mpomvu Mjini Geita.

Tanesco inategemea kuuza Megawati 24 za umeme kila mwezi kwa GGML zenye thamani ya shilingi Bilioni 6 kila mwezi ambao utatumika kwa shughuli za mgodi huo kea uchimbaji na kazi nyingine.

Mgodi huo unatajwa kuendelea kuzalisha umeme wake wenyewe kwa kutumia mafuta ambapo Serikali kupitia Wizara ya Nishati inasema haipati faida kwenye matumizi ya mafuta hayo.

Dkt.Alexander Kyaruzi (katikati) akionyeshwa ujenzi wa katika kituo cha kupozea na kusambaza umeme (substation) cha Mpomvu Mjini Geita, anayemuonyesha ni Mhandisi Dismas Massawe kutoka Tanesco wengine ni wajumbe wa bodi.(Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Kituo hicho cha kupozea na kusambaza umeme cha Mpomvu kinapokea umeme wa msongo wa Kilovoti 220 kutoka Bulyanhulu Kakola.

Dkt.Alexander Kyaruzi amesema kuwa, Tanesco inauza umeme kwenye migodi mingine kama North Mara na Bulyanhulu hivyo GGML haina sababu ya kupata hofu ya kutumia umeme huo badala yake inabidi kujifunza uzoefu wa migodi hiyo inayotumia umeme wa shirika hilo.

Amesema kuwa, Tanesco itapeleka umeme mgodini hapo na GGML itakuwa na wajibu wa kuhakikisha wanafanya jitihada za kuanza kutumia umeme huo mapema.

Mgodi mwingine utakaonufaika na umeme huo ni Stamigold wa Wilaya ya Biharamulo utakaochukua umeme Geita katika kituo hicho cha umeme Megawati 5.

Dkt.Alexander Kyaruzi (wa pili kulia) akikagua sehemu ya mitambo ya umeme katika kituo cha kupozea na kusambaza umeme (substation) cha Mpomvu Mjini Geita,akionyeshwa na Mhandisi Dismas Massawe kutoka Tanesco.(Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Dkt.Alexander Kyaruzi amesema, bodi yake imejiridhisha na maendeleo ya mradi ambao amesema umekamilika kwa kiwango cha asilimia 95 na unawashwa Septemba 16,mwaka huu.

Mhandisi wa Tanesco, Dismas Massawe amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho umekamilika kwa zaidi ya asilimia 95, hivyo mwezi huu watawasha umeme na kuanzia tarehe 18 mwezi huu kila mwananchi anayehitaji umeme huo atakuwa tayari kuomba kuunganishiwa na kupata huduma hiyo.

Mhandisi Dismas Massawe amesema,tatizo la kukatika katika kwa umeme litakuwa limepata ufumbuzi kwa sababu umeme utakuwa unapatikana hapo hapo Geita bila kutegemea kuusafirisha kutoka nje ya Geita.

Amewataka wananchi na wawekezaji kutumia umeme huo kwani utakuwa wa uhakika ambao hautakatika tena.

Massawe amesema kuwa,mradi huo una njia saba za kusambaza umeme ambazo ni kupeleka GGML,Geita,Njia ya kuelekea Mwanza (njia ya Nkome), Stamigold,kwenda kwa wananchi kwa vijiji vinavyopitiwa na mradi.

Bodi ya Tanesco ikiongozwa na mwenyekiti wake,Dkt.Alexander Kyaruzi pamoja na wajumbe wanne wa bodi hiyo, wametembelea miradi mbalimbali katika Mkoa wa Geita kwa siku ya kwanza ambapo imetembelea kituo cha kupozea na kusambaza umeme cha Mpomvu,Stoo ya Tanesco mkoa wa Geita pamoja na ujenzi wa ofisi za Tanesco mkoa wa Geita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news