Vedastus Mathayo Manyinyi:Musoma Mjini tupeni mafiga matatu, tukiingia tu,viwanda vya Prime Catch cha Samaki, Maziwa Musoma vinafufuliwa na haya mengine yote yanatekelezeka kwa wakati

Mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Musoma Mjini,Vedastus Mathayo amesema endapo atashinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, atahakikisha anashughulikia kufufua kiwanda cha Samaki cha Prime Catch kilichopo katika Kata ya Makoko na kiwanda Cha Maziwa cha Musoma ili vifanye kazi hatua ambayo amesema itasaidia kutatua tatizo la ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa Manispaa ya Musoma,anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini), Mara.

Mathayo ameyasema hayo katika Kata ya Makoko alipokuwa akifanya kampeni na kunadi sera za chama hicho ambapo amesema kuwa, atahakikisha viwanda hivyo vinafanya kazi na kuchukua idadi kubwa ya wafanyakazi ambao watapata kipato na kuondokana na tatizo la ajira sambamba na kuboresha Mwalo wa Samaki na dagaa wa Makoko uwe wa kisasa kusudi biashara ifanyike kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, Mathayo ameahidi kutatua changanoto ya huduma ya maji iliyopo katika maeneo ya Zanzibar na Bukanga ambapo amesema atashughulikia haraka iwezekanavyo kwa kushirikiana na Diwani wa CCM, William Gumbo ili waweze kunufaika na huduma hiyo kwa uhakika, sambamba na uwezeshaji wa mikopo kwa wanawake,vijana na walemavu katika kata zote za Manispaa ya Musoma.

Naye Mgombea Udiwani kata ya Makoko ambaye ni Meya wa Manispaa ya Musoma anayemaliza muda wake, William Gumbu, amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ameweza kuboresha barabara ndani ya kata hiyo, kujenga madaraja matatu yanayounganisha Kata ya Buhare pamoja na maeneneo ya Nyamiongo, kujenga sekondari tatu ndani ya kata hiyo, kuongeza vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika baadhi ya shule za msingi zilizokuwa na upungufu, huku shilingi milioni 550 akisema Serikali imekubali kutoa kumalizia uboreshaji wa Kituo Cha Afya cha Makoko.

Gumbo amesema, akichaguliwa atahakikisha anakamilisha ujenzi wa mtaro eneo la Makilagi hadi Zanzibar, kujenga Shule ya mpya ya Msingi katika eneo la Zanzibar pamoja na kuendeleza mtandao wa huduma ya maji katika eneo la Zanzibar na Bukanga ili maeneo yote yaweze kufikiwa na huduma ya maji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini,Benedictor Magiri, amesema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imejitosheleza kukidhi matakwa ya wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini na Watanzania kwa ujumla, kwani masuala yahusuyo huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu, maji, pamoja na miradi mingi ya kiuchumi yameainishwa na hivyo Watanzania wachague viongozi wa CCM kuanzia diwani hadi Rais wakatekeleze ilani hiyo kwa maendeleo ya Watanzania.

"Naomba katika Uchaguzi Mkuu huu, wananchi tuchague viongozi wa Chama Cha Mapinduzi bila kuchanganya, lengo ni kwamba maendeleo yatekelezeke kwa ufanisi diwani akiwa wa CCM na Mbunge wa CCM hadi Rais maendeleo yatapatikana kwa haraka sana kwa umoja tofauti na kuchanganya kutoka vyama vingine ambao watakwamisha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa maslahi mapana ya Wanamusoma na Taifa kwa ujumla,"amesema.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Musoma Mjini Hassan Milanga amesema CCM ndicho chama pekee ambacho kimeendelea kuimarisha amani na umoja wa Kitaifa nchini, na kwamba umoja huo unahitajika kuendelezwa nchini na hivyo ameomba wananchi wa Musoma Mjini kutorubunika kuchagua vyama ambavyo haviwezi kuendeleza amani na kutekeleza dira ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news