Wagombea CHADEMA wanadiwa songea

Watanzania wametakiwa kuendelea kujitokeza kwa wingi katika mikutano mbalimbali ya wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na Urais ili waweze kusikiliza sera na ilani za vyama husika, hatua ambayo itawawezesha kufanya maamuzi sahihi kwa kuchagua viongozi ambao watawaletea maendeleo ifikapo Oktoba 28,mwaka huu, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Hayo yamebainishwa katika mkutano wa kumnadi Mgombea Jimbo la Songea Mjini mkoani Ruvuma, Aden Mayalla pamoja na wagombea udiwani ambapo Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Mbeya, John Mwambigija amewataka wananchi wa jimbo hilo waone umuhimu wa kuchagua wagombea wa upinzani kwani wana ari na nguvu ya kuwatumikia.

Mayalla ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Songea Mjini amesema, iwapo wananchi watampa ridhaa Oktoba 28,mwaka huu atahakikisha anaboresha huduma za afya, elimu, maji, miundombinu.

Sambamba na kuwapatia wazee wote wa Manispaa ya Songea bima za afya pamoja na kuhakikisha kiwanda cha kusindika tumbaku cha SONAMCU kinafufuliwa ili kiweze kutoa huduma na kufungua fursa za ajira.

Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Soko Kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambao ulihudhuriwa na maelfu ya wananchi. Pia amesema kuwa, wananchi wa Jimbo la Songea Mjini wanatakiwa kuwa mfano wa kufanya mabadiliko ya kumchagua mgombea Ubunge Mayalla.

Sambamba na wagombea udiwani ili waweze kushirikiana kwa pamoja kuchochea kasi ya maendeleo ndani na nje ya manispaa hiyo.

Amesema kuwa, huu si wakati wa kugeuzwa mtaji wa baadhi ya wagombea ambao dhamira yao ni kwa ajili ya kutetea maslahi yao.

Mwambigija amewataka wananchi wa jimbo hilo kupuuza maneno yanayosemwa na baadhi ya wanasiasa kuwa endapo wananchi watachagua viongozi toka vyama vya upinzani hawatapata maendeleo.

Amesema kuwa, hoja za wanasiasa hao hazina mashiko huku akisema kuwa majimbo ya Arusha Mjini, Moshi Mjini,Iringa Mjini na Mbeya Mjini yamepiga hatua kubwa kutokana na maamuzi ambayo wananchi waliyafanya huko nyuma.

Rose Mayemba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Njombe amesema, miaka mitano ya wapinzani kutofanya mikutano ya hadhara vyama vyao vimeimarika.

Huku akitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuhakikisha wanakipa chama hicho ushindi wa kishindo kuanzia udiwani, ubunge na udiwani kwani Serikali watakayounda itakuwa daraja baina ya wananchi na mamlaka mbalimbali ili kuwaletea maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news