Wanamgambo wa ADF waua raia 58 DRC

WAZIRI wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Adijo Gidi amesema watu 58 wameuawa na wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya wanamgambo wa ADF wa Uganda katika mkoa wa Ituri Mashariki mwa nchi hiyo.

Gidi pia amesema, idadi kubwa ya watu katika maeneo yaliyoshambuliwa wamekimbia makazi yao wakihofia usalama wao.

Waziri huyo amesema, watu 23 waliuawa katika eneo la mji wa Irumu liliopo Kusini mwa mji wa Ituri.

"ADF iliua watu 23 katika eneo la Irumu Kusini mwa mkoa wa Ituri Jumanne na kisha ikaua watu wengine 35 katika eneo hilo siku iliyofuatia. Vikosi vyetu vimeshafika katika maeneo hayo kukabiliana na wanamgambo hao. Kundi kubwa la watu limeyakimbia makazi yao,"Waziri huyo amekaririwa na AFP.

Aidha, miongoni ma wakazi wa kijiji chenye misitu mikubwa cha Tshabi mkoani hapo amenukuliwa akisema kuwa, wanamgambo hao walitumia bunduki, visu, mapanga na silaha nyinginezo katika mashambulio hayo ya Jumanne na Jumatano.

Mapema mwezi Juni mwaka huu, watu 16 waliuawa na ADF mkoani Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakiwemo watoto 5 wa kike ikiwa ni wiki chache baada ya genge hilo kuua watu wengine 17 katika matukio tofauti mkoani humo.

No comments

Powered by Blogger.