Wizara:Umeme wa uhakika unachochea uwekezaji Geita

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said amesema,kuimarika kwa hali ya umeme mkoani Geita kupitia mradi wa kusafirisha umeme wa Bulyanhulu-Geita na miradi mingine ya usambazaji umeme ya TANESCO, kutachochea shughuli za kiuwekezaji katika miradi ya uzalishaji mali ikiwemo migodi inayotumia umeme mkoani humo, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.

Mhandisi Zena ameyasema hayo alipotembelea banda la TANESCO katika Maonesho ya Teknolojia za Uchimbaji Madini yanayoendelea mkoani Geita  huku TANESCO ikiwa ni mmoja wa wadau wa sekta wezeshi katika maonesho hayo.

Wakati huo huo, Mhandisi Zena ameitaka TANESCO kuendelea kuhamasisha wananchi wengi zaidi kuwekeza katika sekta mbalimbali kama vile migodi, viwanda pamoja na biashara mbalimbali na kuutumia umeme huo kukuza vipato vyao, biashara na uchumi wa Taifa zima kwa ujumla.
Mhandisi Zena Said (wa pili kutoka kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa wataalam wa TANESCO Mkoa wa Geita katika Banda la Maonyesho mjini Geita,wa pili ni Profesa Simon Msanjila Katibu Mkuu Wizara ya Madini.(Diramakini).

"Nimefurahishwa na kasi ya ukamilishaji wa kituo cha kupoza umeme cha Geita. Sasa kazi iliyopo ni kuhakikisha tunahamasisha wateja kuwekeza Geita, hususani wachimbaji wa madini. Kwa kutumia fursa ya umeme wa uhakika ambao sasa upo mkoani Geita,"amesema Mhandisi Zena.

Aidha, ameipongeza TANESCO kwa kazi nzuri ambayo imefanyika katika kuimarisha hali ya upatikanaji umeme mkoani Geita pamoja na maeneo mbalimbali nchini kwa matumizi ya kiuchumi na kijamii na hivyo kuzidi kuchochea kasi ya ukuaji wa kiuchumi na pato la Mtanzania. 

Mhandisi Zena, alipotembelea banda la TANESCO katika maonesho hayo yanayoendelea mkoani Geita, aliambatana na makatibu wakuu wa Wizara za Madini, Katiba na Sheria, Viwanda na Biashara.

Maonyesho ya Teknolojia ya Uchimbaji Dhahabu yanafanyika katika Kijiji Maalum cha maonyesho katika Kituo cha Ukanda maalum kiuchumi (EPZA) mtaa wa bombambili mjini Geita.

Ni mara ya tatu maonyesho hayo yakifanyika katika mji wa Geita ambayo kwa mwaka huu yameanza rasmi Septemba 17 Mwaka huu na yanahitimishwa Septemba 27,mwaka huu.

No comments

Powered by Blogger.